NZEGA YAADHIMISHA SIKU YA KICHAA CHA MBWA DUNIANI KWA KISHINDO, MBWA NA PAKA 14,450 WACHANJWA

Wilaya ya Nzega Mkoani Tabora imeandika historia kwa kuadhimisha kilele cha Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani kwa kishindo, ambapo jumla ya mbwa na paka 14,450 wamechanjwa.Halmashauri ya Nzega ilipewa dozi 21,500 za chanjo ili kufanikisha wiki ya maadhimisho.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo Septemba 28, 2026 katika Viwanja vya Mwanhala, Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai, amesema kila mwananchi ana jukumu la kujilinda na kuwalinda watoto dhidi ya madhara ya ugonjwa huo hatari unaoweza kusababisha kifo kwa binadamu.

"Unapong'atwa na mbwa au kupata mkwaruzo, osha kidonda kwa maji mengi yanayotiririka na sabuni haraka na kisha nenda kituo cha afya. Jamii inapaswa kutoa taarifa mapema kuhusu wanyama wenye dalili hatarishi ili waweze kudhibitiwa," amesema Mhe. Tukai.

Ameongeza kuwa jamii inapaswa kudhibiti mbwa wanaozurura na amewataka wataalamu wa afya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, akisema kaulimbiu ya mwaka huu isemayo "Kwa pamoja tuna nguvu zaidi" ndiyo msingi wa kutokomeza kichaa cha mbwa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Nchini, Dkt. Christopher Sikombe, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, amesema kaulimbiu hiyo inahimiza juhudi za kutokomeza kichaa cha mbwa ifikapo 2030.

Dkt. Sikombe amebainisha kuwa katika wiki ya maadhimisho, zaidi ya watu 6,569 wamepatiwa elimu ya kichaa cha mbwa na ameiomba Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kutumia sheria ndogo katika kudhibiti mbwa wanaozurura.

Naye Dkt. Kennedy Lushasi kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health Institute), amesema taasisi yao itaendelea kushirikiana na Serikali katika tafiti na utoaji wa elimu kwa jamii, huku akisisitiza kuwa chanjo ndiyo kinga pekee na yenye uhakika kwa mbwa na binadamu dhidi ya ugonjwa huo unaoua kwa asilimia 100 pindi dalili zinapoanza kujitokeza.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega Mhe. Naitapwaki Tukai, akizungumza na wananchi wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika leo Septemba 28, 2026 katika Viwanja vya Mwanhala, Wilayani Nzega Mkoani Tabora.

Dkt. Christopher Sikombe, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa Yanayoenezwa na Wadudu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo Nchini, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika leo Septemba 28, 2026 katika Viwanja vya Mwanhala, Wilayani Nzega, Mkoani Tabora.

Dkt. Kennedy Lushasi kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara (Ifakara Health Institute), akizungumza wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yaliyofanyika leo Septemba 28, 2026 katika Viwanja vya Mwanhala, Wilayani Nzega Mkoani Tabora.



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI