MIFUGO NA UVUVI YAHITIMISHA SAFARI YAKE YA SHIMIWI 2026
◼️Yabeba medali ya mchezo wa kurusha Tufe
◼️Kujipanga vema zaidi mwakani
Timu ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliyokuwa ikishiriki michezo mbalimbali kwenye michuano ya SHIMIWI mkoani Kilimanjaro imehitimisha safari yake kwa kubeba medali moja baada ya mchezaji wake Theodata Sallema kuibuka mshindi wa pili kwenye mchezo wa kurusha Tufe.
Timu hiyo ilianza kampeni yake ya kusaka ubingwa wa michezo mbalimbali kwa timu ya mchezo wa kuvuta kamba (wanaume) kufanikiwa kushinda michezo yake yote hatua ya makundi huku upande wa wanawake ikipoteza mchezo mmoja na kutoa sare 1 ambapo timu zote mbili zilifanikiwa kutinga hatua ya mtoano ya 16 bora ya michuano hiyo kabla ya timu ya wanaume kutolewa na timu ya Wizara ya Ujenzi na ile ya wanawake kutolewa na timu ya Mashtaka.
Hata hivyo timu hiyo haikufanya vema kwa upande wa mpira wa miguu ambapo iliishia hatua ya makundi kwa kupoteza mchezo mmoja na kutoa sare michezo yake yote iliyosalia.
Mbali na michezo hiyo, timu hiyo ilikuwa na mshiriki upande wa mashindano ya baiskeli (wanaume) ambapo mwendesha baiskeli wake Siraji Mohammed alimaliza mbio hizo kwa kushika nafasi ya sita huku mchezo wa riadha upande wa mbio ndefu na fupi washiriki wake wakishindwa kuvuka hatua ya pili ya mbio hizo.
Kwa upande wa michezo ya ndani ya karata,bao (wanaume) na bao (wanawake) timu hiyo iliondolewa katika hatua za robo fainali na 16 bora licha ya ushindani mkubwa uliooneshwa na wachezaji wake.
Michuano hiyo ya SHIMIWI inatarajiwa kufanyika tena mwakani mkoani Arusha ambapo Waziri wa habari,Sanaa, Utamaduni na Michezo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Arusha Mhe. Paul Makonda ametangaza utangulizi wa zawadi ya shilingi milioni 500 kwa washindi watakaoibuka kwenye michuano hiyo.


Maoni
Chapisha Maoni