FETA YAHITIMISHA MAFUNZO YA UONGOZI WA JAMII KATIKA UHIFADHI WA RASILIMALI ZA PWANI NA BAHARI
Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Tarehe 27 Septemba, 2026 imehitimisha mafunzo ya muda mfupi ya Uongozi wa Jamii katika Uhifadhi wa Rasilimali za Pwani na Bahari (Conservation Leadership Training Programme) yaliyolenga kuwawezesha viongozi na wadau wa jamii kushiriki kikamilifu katika usimamizi na uhifadhi endelevu wa rasilimali za pwani na bahari.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kampasi ya FETA Mbegani, Bagamoyo, kwa siku 14 kuanzia 14–27 Septemba, 2026 yakishirikisha washiriki 20 kutoka Tanga na Pemba yamefadhiliwa na Ubalozi wa Ireland Tanzania kupitia IUCN Tanzania, huku FETA ikiwa mshirika wa utekelezaji katika kujenga uwezo wa washiriki wanaohusika na usimamizi, matumizi na uhifadhi wa rasilimali za pwani na bahari.
Akifunga mafunzo hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa FETA, Bw. Deus J. Bwathondi, amewataka washiriki kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuleta matokeo chanya katika jamii zao. Alisisitiza kuwa mafunzo hayo hayapaswi kuishia kwa washiriki pekee, bali yawe chachu ya kuwafikia wananchi na vikundi vinavyohusika na matumizi na usimamizi wa rasilimali za pwani na bahari.
“Ninyi mliopata mafunzo haya msiwe walengwa pekee wa maarifa haya. Mnapaswa kuwa walimu na wawezeshaji katika jamii zenu, mkawafikishie wengine ujuzi mliojifunza ili kuongeza uelewa na kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa rasilimali za pwani na bahari,” alisema Bw. Bwathondi.
Aidha amebainisha kuwa FETA itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kujenga uwezo wa jamii katika uhifadhi, usimamizi endelevu na matumizi yenye tija ya rasilimali za pwani na bahari, sambamba na kuchangia utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya taifa na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa IUCN, Bw. Joseph Olila, aliwataka washiriki kuwa mabalozi wa uongozi bora, usimamizi na matumizi endelevu ya rasilimali za pwani na bahari katika maeneo yao. Pia aliipongeza FETA kwa kutoa mafunzo hayo na kusisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa viongozi na wadau wa jamii katika kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari huku akiahidi kuwa IUCN itaendelea kushirikiana na FETA katika shughuli za kujenga uwezo, uhifadhi na maendeleo ya jamii zinazotegemea rasilimali za pwani na bahari.
Katika kipindi cha mafunzo, Washiriki walipatiwa ujuzi kuhusu uongozi wa jamii, uhifadhi wa rasilimali za bahari, usimamizi shirikishi, ufuatiliaji na udhibiti wa shughuli za uvuvi (MCS), usimamizi wa vikundi na vyama vya ushirika, pamoja na usimamizi wa fedha na shughuli za kiuchumi zinazohusiana na rasilimali za bahari. Mafunzo hayo pia yalijumuisha vipindi vya vitendo vilivyowawezesha washiriki kuhusisha maarifa waliyopata na changamoto halisi zinazokabili jamii.




Maoni
Chapisha Maoni