DKT. BASHIRU AAGIZA VIFAA VYA UGANI VITUMIKE KUONGEZA UZALISHAJI WA MAZIWA NCHINI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, leo Oktoba 2, 2026, jijini Dodoma, amekabidhi rasmi magari, pikipiki na vifaa maalumu vya kiufundi vilivyonunuliwa kupitia Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) na kuagiza vifaa hivyo vitumike kuongeza tija ya uzalishaji katika tasnia ya maziwa.

Makabidhiano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha utekelezaji wa mradi na kuhakikisha huduma za kitaalamu zinawafikia wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa haraka, ufanisi na kwa wakati Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo Vifaa vilivyokabidhiwa ni pamoja na Magari 6 aina ya Toyota Hilux Double Cabin; pikipiki 23,  pamoja na vifaa vya ugani.

Akikabidhi vifaa hivyo, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally amesisitiza vifaa hivyo vitumike kwa lengo la kusaidia Walengwa wa mradi na kuleta matokeo chanya katika mageuzi ya Tasnia ya Maziwa nchini Tanzania huku akiwaasa viongozi wa Mikoa iliyokabidhiwa vifaa hivyo kusimamia  uangalizi  makini wa vifaa vyote vilivyo kabidhiwa ili kuleta matokeo chanya kwa walengwa wa mradi.

“Nina waasa viongozi wote wa eneo la mradi, kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya,Kata na vijiji katika mikoa inayo tekeleza mradi huu kusimamia kwa umakini rasilimali hizi ili kuhakikisha zinawanufaisha walengwa wa mradi zikiwemo kaya 140,000 za wafugaji" alisema Mhe. Balozi Dkt. Bashiru.

Naye Waziri wa Kilimo Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Zanzibar, Mhe. Suleiman Masoud Makame ameshukuru kupokea vifaa hivyo na amesisitiza vifaa hivyo vitunzwe na kuhakikisha vinatumika kuleta tija katika tasnia ya maziwa  nchini Tanzania.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bi. Agnes Meena amesema vifaa hivyo vitaongeza uwezo kwa watekelezaji wa mradi kutoa huduma stahiki na kwa wakati kwa wafugaji katika eneo la mradi na hivyo kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa.

C-SDTP ni mpango wa miaka kumi (2024–2034) unaotekelezwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na IFAD, wenye lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ustahimilivu katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kupitia teknolojia zinazozingatia mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuboresha upatikanaji wa masoko, kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi na kupunguza athari za kimazingira katika tasnia ya maziwa.

Waziri Wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Wapili kulia) akikata utepe kuashiria Makabidhiano ya Magari, Pikipiki na Vifaa vya Huduma za Ugani kwa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo Oktoba 02, 2026 Ofisi za Wizara, Mtumba, Dodoma.

Waziri wa Mifugo wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa (Kushoto), Akiendesha Gari Aina ya Hillux Double Cabin ikiwa ni sehemu ya makabidhiano ya Magari, Pikipiki na Vifaa vya Ugani leo Oktoba 02, 2026 .

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji,Maliasili na Mifugo (Zanzibar) Mhe. Suleiman Makame Masoud akiendesha Pikipiki baada ya uzinduzi wa Hafla ya Kukabidhi Magari, Pikipiki na Vifaa vya Ugani kwa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya Maziwa, hafla iliyofanyika Ofisi za Wizara Mtumba, Oktoba 2, 2026 .

Baadhi ya Magari yaliyokabidhiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwa Waratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya  Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi leo Oktoba 02, 2026

Magari na Pikipiki zilizokabidhiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, kwa Waratibu wa Mradi wa Mageuzi ya Tasnia ya  Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi leo Oktoba 02, 2026



Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI