BILIONI 23 ZA MIKOPO ZAFUNGUA FURSA KWA VIJANA - MHE. KAMANI
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepokea Shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia mikopo isiyo na riba katika shughuli za mifugo na uvuvi, na katika awamu ya kwanza, vijana 917 wamenufaika na mikopo hiyo, huku zaidi ya asilimia 52, sawa na vijana zaidi ya 450, wakielekezwa kwenye ufugaji wa kuku, Mpango ambao umelenga kuwaondolea vijana changamoto ya mitaji na kuongeza ushiriki wao katika uzalishaji, usindikaji na biashara za mazao ya mifugo na uvuvi.
Akizungumza katika ufunguzi wa Maonesho ya kumi ya Kitaifa ya ndege wafugwao kwa mwaka 2026 yaliyofanyika leo Oktoba 16, 2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Damas Kamani, amesema Mpango huo unafungua fursa kwa vijana, na mikopo hiyo ambayo imetolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 35 na hutolewa kwa kipindi cha miaka mitano, na uwezeshaji katika ufugaji wa kuku unahusisha ujenzi wa mabanda, ununuzi wa vifaranga, chakula na dawa, pamoja na kuwaunganisha wafugaji na masoko, na amewataka vijana kufuatilia matangazo ya Wizara ili kunufaika na fursa hizo.
“Utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Tasnia ya Kuku wa mwaka 2026–2036 unahitaji uwekezaji wa Shilingi trilioni 3.53 kwa miaka 10, ambapo sekta binafsi inatarajiwa kuchangia asilimia 60, wadau wa maendeleo asilimia 25 na serikali asilimia 15, na Mkakati huo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya kuku katika pato la taifa kutoka asilimia 1.8 hadi asilimia 3, kuongeza uzalishaji wa mayai kutoka bilioni 7.1 hadi bilioni 17.3 kwa mwaka na nyama ya kuku kutoka tani 156,000 hadi tani 380,000, na serikali pia imeweka Shilingi bilioni 300 katika benki kwa ajili ya mikopo yenye riba nafuu kwa wakulima na wafugaji”. amesema Mhe. Kamani
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Fabian Magawa Madele, amesema mafanikio ya maonesho hayo yanapaswa kuonekana kupitia biashara, uwekezaji na ushirikiano wenye matokeo yanayopimika, na maonesho ya mwaka huu yamevutia waoneshaji 72 kutoka ndani na nje ya nchi, yakitoa fursa ya kubadilishana teknolojia na uzoefu, na pia amehimiza taasisi za fedha kuongeza ushiriki katika kutoa mitaji na wakulima kuongeza uzalishaji wa soya na mahindi yanayotumika kutengeneza chakula cha kuku.
Naye, Mwakilishi wa Chama cha Wafugaji Kuku cha Tanzania (PAT), Bw. Sufian Zuberi Kyarua, amesema wafugaji bado wanakabiliwa na gharama kubwa za chakula na ugumu wa kupata mikopo yenye riba nafuu, na ameomba serikali kuimarisha utafiti wa kupunguza gharama za uzalishaji, kupanua mikopo kwa wadau wote na kuongeza bajeti pamoja na wataalamu wa sekta hiyo, na amependekeza mayai kuingizwa katika programu za chakula shuleni ili kila mwanafunzi apatiwe angalau mayai matatu kwa wiki, akisisitiza umuhimu wake katika kuboresha lishe ya watoto.
















Maoni
Chapisha Maoni