Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Edwin Mhede ameitaka Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kuongeza uzalishaji wa vifaranga vya samaki ili viweze kukidhi hitajio kubwa lililopo hapa nchini.
Dkt. Mhede ametoa kauli hiyo jana, 29 Januari 2026 alipotembelea FETA Kampasi Kuu ya Mbegani kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na FETA pamoja na miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
"Niwapongeze kwa utotoleshaji huu wa vifaranga na ufugaji samaki kwa ujumla ila niwasihi muongeze zaidi kasi ya uzalishaji vifaranga ili viende maeneo yenye uhitaji na nyie kujipatia kipato" amesema Dkt. Mhede.
Aidha, ameishauri FETA kuwekeza katika ufugaji samaki (hasa kwenye vizimba) katika maeneo mbalimbali ikiwepo Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa lengo la kutoa mafunzo zaidi kama mashamba darasa na pia uzalishaji wa biashara ili kuongeza mapato.
Awali Mtendaji Mkuu wa FETA, Dkt. Semvua Mzighani amesema kuwa kwasasa FETA inaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu katika ufugaji wa samaki ili wananchi na Taifa kwa ujumla lifaidike zaidi na fursa zilizopo katika Uchumi wa Buluu. Maeneo ya kipaumbele ni pamoja na: ufugaji samaki, ufugaji wa Tango (Jongoo) Bahari, unenepeshaji wa Kaa na kilimo cha Mwani.
Akiwa FETA Dkt. Mhede alipata fursa ya kujionea mazingira mbalimbali ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo eneo la utotoleshaji wa vifaranga vya samaki, mabwawa ya kufugia samaki aina ya sato na kambale, eneo la kukaushia samaki na mwani, Zahanati na Idara ya Uvuvi na Ubaharia ambapo alipata fursa kuongea na wanafunzi wa Fani ya Uvuvi na Ubaharia.







Hakuna maoni:
Chapisha Maoni