Nav bar

Jumatano, 4 Februari 2026

BILION 7 KUKWAMUA VIJANA KIUCHUMI KUPITIA UFUGAJI SAMAKI

Wizara ya Mifugo na Uvuvi ,imetenga shilingi bilioni 7 katika mwaka wa fedha 2025/2026 Kwa lengo la kuwezesha vijana kupata mitaji kupitia mikopo yenye masharti nafuu, fedha zitakazo wanufaisha vijana 308 waliopatiwa mafunzo ya ufugaji wa samaki.

Hayo yamesemwa   Februari 3, 2026, Bungeni Jijini Dodoma na Naibu  Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Ng’wasi Kamani  wakati akijibu swali la mbunge wa Bukoba Vijijini Mhe. Dkt. Jasson Samson Rwekiza aliyetaka kufahamu kuhusu mikopo ya vizimba vya samaki ili kukuza uchumi ambapo  amesema katika awamu ya kwanza Serikali ilitoa mikopo ya vizimba 44 yenye thamani ya shilingi milioni 986.80 katika Mkoa wa Kagera ambapo wanufaika 101 walinufaika na mpango huo.

Aidha, Mhe. Kamani amesema, Serikali imeanza utekelezaji wa ahadi ya Mhe. Rais ya kutenga shilingi bilioni 200 kwa ajili ya mikopo ya vizimba ndani ya siku 100, hatua itakayoongeza fursa kwa vijana katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Bukoba na Musoma.

"Serikali imetoa mikopo ya vizimba 47 yenye thamani ya shilingi bilioni 1.126 kwa wafugaji wa samaki wa vizimba  Musoma Mjini, ambapo wanufaika 130, wengi wao wakiwa vijana, walipata mikopo hiyo bila riba." Mhe. Kamani

Aliongeza kuwa Wizara inaendelea kutekeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT–Uvuvi) kwa kutoa mafunzo, vitendo na mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana ili kuongeza uzalishaji, kipato na ajira katika sekta ya uvuvi.

Hata hivyo, Mhe. Kamani, aliomba ridhaa ya Bunge kuendelea kutekeleza mpango wa kutenga asilimia 10 ya mikopo ya uvuvi kwa ufugaji wa samaki wa vizimba katika maeneo yenye fursa ya shughuli hiyo, sambamba na kuendelea kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kuongeza idadi ya wanufaika nchini.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni