Na Daudi Nyingo – Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefungua milango ya uwekezaji kwa wafanyabiashara kutoka Oman, hatua inayolenga kuimarisha diplomasia ya kiuchumi iliyojengwa baina ya nchi hizo mbili kwa muda mrefu.
Ujumbe wa wafanyabiashara hao kutoka Oman ulioongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara na Viwanda katika Mkoa wa Al Wusta na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Biashara na Viwanda cha Oman, Dkt. Salem Al-Junaibi (Mb), uliokutana Septemba 9, 2025 na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiongozwa na Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Prof. Mohamed Sheikh, katika ukumbi wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Temeke jijini Dar es Salaam.
Mazungumzo hayo yalijikita katika kuangalia fursa za kuwekeza kwenye maeneo ya uchakataji wa nyama na samaki, ujenzi wa viwanda vya ngozi na maziwa, ufugaji wa kisasa wa samaki, uzalishaji wa chakula cha mifugo, uzalishaji wa chanjo za mifugo, pamoja na miradi ya baridi (cold chain facilities) kwa ajili ya kuhifadhi na kusafirisha mazao ya mifugo na uvuvi kwenda masoko ya kimataifa.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Oman uliambatana pia na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdalah Kilima.






Hakuna maoni:
Chapisha Maoni