Nav bar

Ijumaa, 4 Julai 2025

RAIS SAMIA ANAWAPENDA WAFUGAJI-DKT. KIJAJI

Na. Omary Mtamike

◼️Takribani mifugo 4281 yachanjwa mkoani Arusha

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuidhinisha kiasi cha Bil. 216 kwa ajili ya ruzuku ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo kimedhihirisha mapenzi makubwa aliyonayo kwa wafugaji waliopo nchini.

Mhe. Dkt. Kijaji amesema hayo Julai 03, 2025 Wilayani Ngorongoro wakati akihitimisha ziara yake ya ukaguzi wa utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya chanjo na utambuzi wa Mifugo katika mkoa wa Arusha ambapo takribani Mifugo 4281 imetambuliwa na kuchanjwa.

“Tayari Mhe. Dkt. Samia ameshatoa Bil. 65 zitakazotumika kwa ajili ya zoezi hilo kwa mwaka huu hivyo wafugaji tunaenda kunufaika na mifugo yetu kwa sababu tayari kuna soko linalohitaji tani Elfu 50 za nyama inayotokana na mifugo yetu iliyochanjwa na kutambuliwa” Amesema Mhe. Dkt. Kijaji.

Aidha Mhe. Dkt. Kijaji amebainisha kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa miaka 5 wa uboreshaji sekta ya Mifugo ulioasisiwa na Mhe. Rais Samia katika kuhakikisha maisha ya wafugaji yanabadilika kupitia ufugaji wa kisasa unaoendana na matakwa ya soko la kimataifa.

Ziara hiyo ya Mhe. Dkt. Kijaji iliyolenga kukagua utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo iliyozinduliwa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu Juni 16, 2025 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea katika mikoa ya Mara, Simiyu, Geita, Pwani, Morogoro, Tabora na Dodoma.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akitoa chanjo ya Ugonjwa wa mdondo wa kuku wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi la Kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Julai 03, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akishuhudia namna zoezi la uchanjaji mifugo linavyofanyika wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi hilo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Julai 03, 2025.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji akioneshwa namna mfumo wa utambuzi wa Mifugo kielektroniki unavyofanya kazi wakati wa ziara yake ya Ukaguzi wa utekelezaji wa zoezi la Kampeni ya kitaifa ya Chanjo na Utambuzi wa Mifugo Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha Julai 03, 2025. Kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Kenan Kihongosi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni