Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti amesema serikali inaendele kutekeleza mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa lengo la kuhakikisha afya za watoto zinaendelea kuimarika.
Naibu Waziri Mnyeti ameyasema hayo leo
(27.09.2023) wakati akihitimisha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni
yaliyofanyika katika viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza. Mnyeti amesema
serikali imedhamiria kuhakikisha watoto wanakuwa na lishe bora hivyo ni lazima
itekeleze mpango wa unywaji maziwa shuleni kwa kuwa maziwa ni muhimu katika
kuboresha afya za watoto.
Siku ya unywaji maziwa shuleni ni muhimu na ina lengo la kutoa
hamasa ya kuboresha afya za watoto shuleni kupitia matumizi ya maziwa na bidhaa
zake. Wataalamu wa lishe wanashauri kuwapa watoto mlo ulio bora zaidi na wenye
kutoa virutubisho vyote muhimu na maziwa yamethibitika kuwa chakula muhimu
zaidi kwa watoto na hata kwetu watu wazima.
“Watalaamu wetu wa lishe wanashauri kuwa mtoto wa shule (msingi na
sekondari) apewe angalau glasi moja ya maziwa kila siku na itapendeza kama
maziwa yatatolewa shuleni ili kumpa nguvu mtoto wakati akiendelea na masomo,”
amesema
Naibu Waziri Mnyeti amesema kuwa watoto wengi nchini wakiwemo wa Mkoa wa Mwanza
huondoka nyumbani asubuhi 3 kwenda shuleni bila kupata chakula chochote. Aidha,
shuleni nako mara nyingi hawapati chakula na hivyo kuwafanya watoto kuwa na
njaa, kukosa usikivu mzuri, na baadaye kutoona faida ya masomo.
Maziwa husababisha watoto kukua vizuri kimwili na kiakili hivyo
yakitolewa kwa shuleni yataleta maendeleo mazuri kiakili na kimwili kwa watoto
na siku za usoni tutakuwa na Taifa lenye watu wazuri walio na uelewa mkubwa. Ni
muhimu kufanya hivi ili kuandaa Taifa lililo bora siku zote lakini kuwa na
watoto wenye uelewa mkubwa.
“Nitoe wito, Wakurugenzi, wataalam wetu katika Halmashauri zote
sasa tuendelee kwa kasi kuhamasisha, tuwape Maziwa watoto na tufuatilie
maendeleo yao, mipango mizuri ifanyike 4 kuhakikisha watoto wanapata maziwa
shuleni. Hata katika mpango wa lishe, maziwa iwe sehemu ya mlo wa mwanafunzi,”
amesema
Naibu Waziri Mnyeti amewasihi wadau
wa Sekta Binafsi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha Watoto wanapata
maziwa shuleni ili kuinua viwango vyao vya ufaulu.
Inahitajika miundombinu na nguvu ya kusambaza maziwa shuleni hivyo ni vyema
wadau wote kwa pamoja kujipanga kwa dhati kabisa ili kufanikisha jambo hilo.
Aidha, wafugaji wametakiwa kuzalisha maziwa kwa wingi na wasindikaji na wadau
wametakiwa kuhakikisha wanajisajili kwenye Bodi ya Maziwa Tanzania ili waweze
kutambulika.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imeendelea kuwekeza mazingira mazuri katika kuendeleza Tasnia ya Maziwa nchi.
Kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imefanikiwa kutoa mikopo yenye
thamani ya Tsh 1.02 Billion kwa ajili ya ununuzi wa Ng’ombe bora wa Maziwa 398
kwa wafugaji wadogo wa Maziwa kupitia AMCOS & VIkundi ya uzalishaji Maziwa
ili kuongeza uzalishaji wa Maziwa hapa nchini. Pia serikali kupitia TADB Mradi
wa TI3P imeweza kutoa ruzuku ya 25% ya gharama za Mitamba yenye thamani Tsh
257,256,625 ili kumpunguzia Mzigo wa Gharama za uendeshaji kwa mfugaji mdogo
ili aweze kufuga kwa tija.
“Tutumie fursa hii aliyotupatia Mhe Rais kuongeza uzalishaji na
usindikaji, tuimarishe ubora wa maziwa ili tuwe na maziwa mengi yaliyosindikwa.
Watu wanaouza maziwa mitaani wasilianeni na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB),
nunueni vifungashio, uzeni maziwa salama, ili maziwa yatupatie afya yasituletee
madhara. Wananchi kunyweni maziwa yaliyosindikwa, watoto kunyweni maziwa,
Wizara inawezesha, maziwa yanapatikana,” amesema
Naibu Waziri Mnyeti amewashukuru Bodi
ya Maziwa Tanzania (TDB), Katibu Tawala Mkoa wa
Mwanza, Wakurugenzi wa Halmashauri, Watendaji wa Serikali, Benki ya Maendeleo
ya Kilimo (TADB), Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Gain Tanzania, Heifer
International, ASAS Dairies LTD, Galaxy Food, Yoba for Life Foundation, wasindikaji
wote wa kanda ya ziwa na wananchi kwa kuandaa, kushiriki na kufanikisha madhimisho
hayo.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. AminaMakilagi akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza amesema kwa upande wa mkoa walikuwa wakiendelea na utekelezaji wa mpango
wa utoaji wa chakula shuleni hivyo kutokana na umuhimu wa maziwa latika kukuza
lishe kwa Watoto watahakikisha suala la unywaji maziwa shuleni nalo linapewa
kipaumbele ili kuhakikisha Watoto wanakuwa na afya bora.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Ushauri ya TDB, Prof. Zacharia Masanyiwa amewasihi wazazi na walezi
kuhakikisha Watoto wanapata lishe iliyo bora ambayo inapatikana kupitia
matumizi ya maziwa. Aidha, ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Mifugo na
Uvuvi kwa namna wanavyoiwezesha Bodi ya Maziwa kutimiza majukumu yake katika
kuwahudumia watanzania.
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB),
Dkt. George Msalya amewasihi wafugaji kuhakikisha wanapeleka maziwa yao kwenye
vituo vya kukusanyia maziwa ili yaweze kupimwa ubora wake kabla ya kwenda kwa
walaji. Pia amewasihi wananchi kutumia maziwa ambayo yamesindikwa kwa kuwa ni
salama.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni “Mpe Mtoto Maziwa kwa Maendeleo Bora Shuleni”, ikiwa na lengo
la kuwa na Taifa lenye watoto wenye afya bora na uelewa wa juu sana na hivo
kusaidia nchi kupata maendeleo zaidi. Wazazi na Walimu kwa pamoja tushirikiane
kuwapa watoto maziwa yaliyosindikwa wawapo shuleni na nyumbani.
Pamoja na kuhitimisha maadhimisho hayo,
Mnyeti pia amezindua Kituo cha Uhimilishaji Kanda ya Ziwa ambacho mtambo wake
wa kuzalisha hewa baridi ya naitrojeni ulikuwa umeharibika toka mwaka 2016
lakini baada ya matengonezo yaliyofanyika mwaka 2023 sasa unafanya kazi vizuri.
Kituo hicho kunafanya kazi ya kuhifadhi
na kusambaza mbegu bora za mifugo zinazozalishwa katika Kituo cha Taifa cha
Uhimilishaji (NAIC) kilichopo mkoani Arusha. Kwa sasa kituo hicho kinatoa
huduma ya uhimilishaji kwenye mikao ya Kanda ya Ziwa pamoja na mikoa jirani ya
Katavi, Tabora na Kigoma. Kwa mwaka huu wa fedha hadi kufikia 26 Septemba 2023
jumla ya mirija 3,207 ya mbegu imesembazwa.
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) akiongea na wananchi wa Jiji la wa Mwanza wakati akihitimisha Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha. Mhe. Mnyeti amewasihi wazazi na viongozi kuhakikisha wanausimamia mpango huo wa unywaji maziwa shuleni kwa kuwa maziwa yanawasaidia Watoto kuwa na lishe bora. (27.09.2023)
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) akimsikiliza mmoja wa wadau wa usindikaji maziwa (kushoto) waliofika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza. (27.09.2023)
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) akifurahi pamoja na watoto wa shule ambao walifika kwenye Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza mara baada ya kugawa maziwa. (27.09.2023)
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) akitoa zawadi ya begi la shule kwa mmoja wa wanafunzi ambao walishinda mashindano ya insha na taaluma wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza. (27.09.2023)
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TDB, Prof. Zacharia Masanyiwa akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Furahisha Jijini Mwanza ambapo amewasihi wazazi na walezi kujali afya za Watoto kwa kuhakikisha wanapata lishe bora inayopatikana kupitia unywaji wa maziwa. (27.09.2023)
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Dkt. George Msalya akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Unywaji Maziwa Shuleni ambapo amewasihi wananchi kuhakikisha wanatumia maziwa ambayo ni salama. Pia amewasihi wafugaji kuhakikisha wanavitumia vituo vya kukusanyia maziwa ili maziwa hayo yaweze kupimwa ubora na pia kupelekwa kwenye viwanda kwa ajili ya kusindikwa. (27.09.2023)
Mwakilishi wa wafugaji na mnufaika wa Mkopo wa ununuzi Ng'ombe wa maziwa na Ruzuku ambaye ni Mwenyekiti wa UWAKO AMCOs cha Korogwe mkoani Tanga na Makamu Mwenyekiti wa TDCU akipokea Nakala ya Hundi iliyotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa niaba ya wafugaji na Vyama nufaika kutoka kwa Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb). (27.09.2023)
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mhe. Amina Makilagi (wa pili kutoka kulia) akitoa taarifa ya hali ya Sekta ya Mifugo na Uvuvi kwa mkoa wa Mwanza wakati Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) alipotembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kusaini kitabu cha wageni. (27.09.2023)
Afisa Mfawidhi wa Kituo cha Uchunguzi wa Magonjwa ya Wanyama Kanda ya Ziwa, Sr. Rosamystica Sambu akitoa utambulisho wa watumishi waliopo kwenye Taasisi za Wizara kwa Kanda ya Ziwa (hawapo pichani) wakati Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) alipofika Mwanza kwa ajili ya kuzindua kituo cha Uhimilishaji kwa Kanda ya Ziwa. (27.09.2023)
Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti (Mb) akihoji jambo na kupata maelezo kutoka kwa Msimamizi wa Kituo cha Uhimilishaji Kanda ya Ziwa, Abdallah Thabit (kulia) wakati alipofika kituoni hapo kwa ajili ya kukizindua. Katikati ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC), Dkt. Dafay Bura. (27.09.2023)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni