#MifugoNaUvuviNiUtajiri
Alhamisi, 31 Agosti 2023
WALIOCHOCHEA MGOGORO WA WAKULIMA NA WAFUGAJI LINDI KUKIONA
◾ Silinde na Sagini wacharuka!
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini wameamuru kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria wale wote waliohusika kwenye mauaji yaliyotokana na mgogoro wa wafugaji na wakulima kwenye kijiji cha Ngunichile wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.
Viongozi hao wamebainisha hayo leo Agosti 30, 2023 muda mfupi baada ya kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuona hali halisi ya mgogoro huo ambapo wamevitaka vyombo vya usalama kuwakamata watuhumiwa wote wa mauaji yaliyotokana na mgogoro huo na kuwafikisha mahakamani.
"Wakulima na wafugaji wote ni Watanzania na ni wajibu wetu kama viongozi na watendaji kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na ndio maana Mhe. Rais Dkt. Samia ametuamini na kutuweka katika nafasi tulizonazo" Ameongeza Mhe. Silinde.
Aidha Mhe. Silinde amebainisha kuwa uchunguzi wake umebaini migogoro hiyo inachochewa na baadhi ya Viongozi wasio waaminifu kutoka ngazi za kata na vijiji ambao mara nyingi wamekuwa wakiwaruhusu wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye maeneo wasiyoruhusiwa.
"Katika kuhakikisha tunakomesha kabisa migogoro ya aina hii Septemba Mosi mwaka huu uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na sekretarieti yake yote utakutana na wakuu wa Mikoa yote ya Kusini na ile ya Pwani ili kujadili taarifa ya kikosi kazi tulichokiunda na hatimaye tutoke na maazimio ya pamoja yatakayotekelezwa na pande zote" Ameongeza Mhe. Silinde.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa mambo ya ndani Mhe. Jumanne Sagini amewataka wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wamekimbia makazi yao kwa kuhofia hali ya usalama warejee na kufanya shughuli zao kama kawaida.
"Serikali ya Dkt. Samia kamwe haiwezi kuacha watu wakimbie makazi yao kwa kuhofia usalama wao na kama hali hiyo itaendelea maana yake hata sisi aliotuamini kulinda raia na mali zake hatutoshi kwenye nafasi zetu" Amesema Mhe. Sagini.
Mhe. Sagini amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa kijiji hicho kulinda amani wakati wote na kuwa vinara wa kutoa taarifa pale wanapohisi jambo lolote linaloashiria uvunjaji wa amani.
Hivi Karibuni kumeibuka migogoro baina ya wafugaji na wakulima mkoani Lindi huku chanzo kikubwa cha migogoro hiyo kikiwa ni uvamizi unaofanywa na wafugaji kwenye baadhi ya maeneo ya wakulima.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Agosti 30, 2023 muda mfupi kabla ya kuelekea kwenye kijiji cha Ngunichile kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohammed Moyo muda mfupi baada ya kuwasili wilayani hapo Agosti 30, 2023 kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye kijiji cha Ngunichile.
Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi Agosti 30, 2023 alikofika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Nachingwea.
ULEGA AFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MSAFARA KUTOKA TAASISI YA WORLDLINE YA UFARANSA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akiongea na Mkuu wa msafara kutoka taasisi ya Worldline ya Ufaransa, Bi. Caroline Jesequel (wa pili kutoka kushoto) alipofika ofisini kwa Waziri huyo jijini Dar es Salaam leo Agosti 28, 2023. Lengo la ziara ya Bi. Jesequel na wenzake ni kujitambulisha na kujenga mazingira ya ushirikiano baina yao na Wizara katika kuboresha mfumo wa utambuzi na takwimu za mifugo. Wa tatu kutoka kulia ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe. Wa kwanza kulia ni Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Daniel Mushi. Wa kwanza kushoto ni Mtaalam wa masuala ya ushirikiano wa kimkakati kutoka Worldline, Bi. Yulia Kostenko.
Ujumbe kutoka taasisi ya Worldline ya Ufaransa ukiongozwa na Bi. Caroline Jesequel (wa kwanza kulia) wakifuatilia wasilisho kuhusu taarifa ya ufuatiliaji na utambuzi wa mifugo katika kikao kilichofanyika kwenye Ofisi za Wizara zilizopo jijini Dar es Salaam leo Agosti 28, 2023. Wa kwanza kushoto ni Mtaalam wa Mifumo ya Utambuzi ya masuala mbalimbali, Bw. Sebastien Spanneut. Katikati ni Mtaalam wa masuala ya ushirikiano wa kimkakati, Bi. Yulia Kostenko.
Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga akiwasilisha taarifa kuhusu ufuatiliaji na utambuzi wa mifugo Wakati wa kikao baina ya Wageni kutoka taasisi ya Worldline ya Ufaransa na Viongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kilichofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 28, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (kulia) akisalimiana na Mkuu wa msafara kutoka taasisi ya Worldline ya Ufaransa, Bi. Caroline Jesequel alipofika ofisini kwa Waziri huyo jijini Dar es Salaam leo Agosti 28, 2023. Lengo la ziara ya Bi. Jesequel na wenzake ni kujitambulisha na kujenga mazingira ya ushirikiano baina yao na Wizara katika kuboresha mfumo wa utambuzi na takwimu za mifugo. Katikati ni Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe.
WAZIRI ULEGA ANADI FURSA ZA AJIRA SEKTA ZA MIFUGO NA UVUVI KWA WAKUU WA MIKOA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amewahimiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa zilizopo kwenye sekta za mifugo na uvuvi ili waweze kujiongezea kipato na kujikwamua kimaisha.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala muda mfupi baada ya kutoa mada kuhusu fursa za ajira zinazopatikana kwenye sekta ya mifugo na Uvuvi wakati wa mafunzo ya uongozi kwa Viongozi hao yanayoendelea kufanyika kwenye shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani Agosti 26, 2023.
Sehemu ya Wakuu wa Mikoa wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (hayupo pichani) wakati alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu fursa za ajira zinazopatikana kwenye sekta ya mifugo na Uvuvi wakati wa mafunzo ya uongozi kwa Viongozi hao yanayoendelea kufanyika kwenye shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha, Mkoani Pwani Agosti 26, 2023.
Jumanne, 29 Agosti 2023
Jumapili, 27 Agosti 2023
WAZIRI ULEGA AELEZA MIKAKATI YA UKUZAJI CHAKULA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wamejizatiti kuhakikisha Tanzania inakuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo leo Agosti 22 jijini hapa alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya wahariri na waandishi wa habari, ikiwa ni maandalizi ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linalotarajiwa kufanyika Septemba.
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwani tayari tumeanza na BBT LIFE (Building a Better Tomorrow- Livestock and fisheries Enterpreneurs), ili tuwe na uzalishaji mkubwa.
"Tuna vijana 700 wanaofundishwa kule Tanga, Mwanza na Kagera," alisema.
"Sasa kuna fedha za mabadiliko ya tabia nchi, ambazo mkulima anaweza kulima majani ya mifugo ambayo yatasaidie kuondoa hewa ukaa na kufanya biashara.
"Tunaitaka bandari ije haraka ili tusafirishe mifugo, tutasafirishe mbuzi, maana wengine wanataka wachinje wenyewe. Sio tunavutana tu, tunataka mambo yatokee haraka," amesisitiza.
Kuhusu masoko, amesema yatapatikana kwani uzalishaji unaendelea kuongezeka.
"Tumenunua ndege inayoweza kubeba tani 60, ambazo ni sawa na kiwanda kimoja tu cha samaki pale Mwanza.
"Katika msimu wa 2021, tuliuza tani 1,724; Mwaka 2022/ 23 tumeuza tani 14,000, kwa hiyo tunaomba ushirikiano wenu," amesema.
Kuhusu AGRF, Waziri Ulega amesema awali sekta za mifugo na uvuvi hazikuwepo, lakini katika mkutano uliofanyika Kigali nchini Rwanda, sekta hizo ziliingizwa.
"Kwa mara ya kwanza mkutano huu unafanyika nchini ukiwa na mifugo na uvuvi.
Ujio wa mkutano huo ni fursa adhimu, tunataka tuilishe dunia kupitia kilimo. Kauli mbiu yetu ni 'vijana na wanawake ndio kiini cha uzalishaji."
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Taasisi ya Kilimo ya Afrika (Aggra), Vianey Rweyendela amesema Tanzania imepata fursa kubwa kwankuwa na mkutano wa AGRF.
"Huu ni wakati wetu kuitangaza nchi yetu. kwa sasa tunaelekea kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
"Hakuna nchi iliyokwepa umasikini lakini kupitia kilimo tunaweza kujikwamua. Kwa uchambuzi tumeufanya, tumesema tusipotenga Sh5 trilioni kwenye wizara zinazohusika na kilimo, hatutatoka kwenye umasikini," amesema.
Naye mwakilishi wa taasisi ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Dk James Rao amesema elimu zaidi inahitajika kuelewa umuhimu wa mifugo kwa lishe na uchumi.
"Miaka michache iliyopita mifugo ilipewa jina baya la kuharibu mazingira, wakisema inazalisha hewa ukaa, lakini ukweli ni kwamba inachangia kuboresha mazingira na hili linapaswa kuelezwa," amesema.
"Mifugo inachangia asilimia 40 katika mazao ya kilimo na sehemu nyingine hadi asilimia 80. Inachangia kuboresha lishe, ajira na malighafi za bidhaa.
Mbali na wataalamu na waandishi wa habari, mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salim Mtambile.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea wakati akifungua mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea mkutano wa AGRF utakaoanza Septemba 5 hadi 8, 2023. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Daniel Mushi akitoa neno la utangulizi kabla ya ufunguzi wa mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea mkutano wa AGRF. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wahariri na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kufungua Mafunzo kwa wahariri hao kuelekea mkutano wa AGRF. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
SILINDE AONGOZA MAPOKEZI YA TANI 25.8 ZA SAMAKI WASIOLENGWA
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde leo Agosti 20, 2023 ameongoza mapokezi ya tani 25.8 ya samaki wasiolengwa au "bycatch" kama inavyojulikana kitaalam ambao wamevuliwa katika ukanda wa bahari kuu.
Katika hafla ya mapokezi ya samaki hao wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 85 za kitanzania iliyofanyika Wilaya ya Mwanakwerekwe visiwani Zanzibar Mhe. Silinde ameipongeza kampuni ya "Albacora" inayomiliki meli ya "Pasific Star" kwa kuanza kutekeleza sehemu ya makubaliano baina yake na mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ambapo Meli hiyo itakuwa ikishusha kiasi cha tani 100 za samaki wasiolengwa kila mwaka.
"Samaki hawa tulioanza kuwapokea leo wataongeza mapato ya Serikali kupitia chanzo hiki kipya, usalama wa chakula na lishe na kutokana na wingi wa samaki watakaokuwa wakishushwa nina uhakika hata bei ya samaki hapa nchini itapungua na hivyo kuwawezesha wananchi wengi hususan wenye kipato cha chini kumudu gharama za bidhaa hii" Amesema Mhe. Silinde.
Mhe. Silinde ameongeza kuwa hatua hiyo pia itaimarisha biashara ya samaki hasa kwa wanawake ambao wamekuwa wakijihusisha na ununuzi na uuzaji wa samaki nchini na hivyo kuboreshw mnyororo wa thamani wa bidhaa hiyo kwa ujumla.
"Serikali inayoongozwa na mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya jitihada nyingi sana katika kuimarisha sekta ya Uvuvi na kuongeza mapato yatokanayo na sekta hiyo kwa ujumla hivyo tunategemea uvuvi wa bahari kuu utakuwa ni moja ya chanzo kikubwa sana cha mapato nchini " Amesisitiza Mhe. Silinde.
Aidha Mhe. Silinde ameipongeza kampuni ya Albacora kwa kuanza utekelezaji wa makubaliano yake na Mamlaka ya wa bahari kuu ambapo amesema kuwa Serikali inataka wawekezaji wa aina hiyo na hivyo kuiomba Mamlaka hiyo kuendelea na jitihada za kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Meli ya "Pasific Star" inayomilikiwa na kampuni ya Albacora imepewa kibali cha kuvua samaki katika ukanda wa bahari kuu ikiwa ni moja ya hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutekeleza dhana kwa vitendo dhana ya uchumi wa buluu.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar Mhe. Suleiman Makame (katikati), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kutoka Tanzania Bara Mhe. David Silinde (kulia kwake) wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu na wale wa meli ya Pasific Star muda mfupi baada ya mapokezi ya Tani 25.8 za samaki wasiolengwa yaliyofanyika leo Agosti 20, 2023 Mwanakwerekwe Zanzibar.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu Dkt. Emmanuel Sweke wakifuatilia jambo wakati wa hafla ya mapokezi ya Tani 25.8 za samaki wasiolengwa yaliyofanyika leo Agosti 20, 2023 Mwanakwerekwe Zanzibar.
Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi kutoka Zanzibar Mhe. Suleiman Makame (kushoto), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kutoka Tanzania bara Mhe. David Silinde (wa pili kutoka kulia), Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Khamis Mwalimu, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uvuvi wa bahari kuu Dkt. Emmanuel Sweke (aliyevaa kofia) wakiwa wameshika baadhi ya samaki wasiolengwa ikiwa ni ishara ya mapokezi ya Tani 25.8 za samaki hao yaliyofanyika leo Agosti 20, 2023 Mwanakwerekwe Zanzibar.
MAFUNZO YA UFUGAJI MAJONGOO BAHARI YATOLEWA WILAYANI BAGAMOYO
Ufugaji wa Jongoo Bahari Kaole - Bagamoyo
Shamba la Jongoo Bahari Kaole - Bagamoyo
WAZIRI ULEGA AFANYA MAZUNGUMZO NA MBUNGE WA AFRIKA MASHARIKI MHE. JAMES OLE MILLYA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega(Mb) amekutana Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. James Ole Millya, na kufanya mazungumzo kuhusu Maendeleo ya sekta ya Mifugo, mazungumzo hayo yamefanyika ofisini kwake Jijini Dodoma, Agosti 17,2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akiwa katika picha ya pamoja na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. James Ole Millya, alipoenda kumtembelea ofisini kwake jijini Dodoma Agosti 17,2023.
UFUGAJI WA SAMAKI CHANZO MBADALA CHA KIPATO KWA WAVUVI - ULEGA
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali inaweka msisitizo mkubwa katika ufugaji wa kisasa wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuwawezesha wavuvi kuwa na chanzo mbadala cha kipato na kupunguza utegemezi wa shughuli za uvuvi katika maji ya asili.
Mhe. Ulega ameyasema hayo Agosti 16, 2023 wakati wa kufungua Kongamano la wadau la kujadili Sera, Sheria na kanuni za Uvuvi za kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika
Amesema kwamba lengo la Serikali ni kuweka nguvu kubwa katika ufugaji wa samaki ili kuacha maji ya asili yaweze kupumua na kuondoa wasiwasi wa kipato kwa wavuvi kila siku
"Mtu akiwa na vizimba vyake na kufuga samaki vizuri na kuwapeleka sokoni ana uhakika wa kupata kipato Alisema Mhe. Ulega
Aidha ameongeza kuwa katika jitihada hizo za Serikali ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kulinda rasilimali za uvuvi huku akiongeza kuwa ni muhimu wadau wenyewe wakujua ulinzi wa rasilimali ni jambo lao wenyewe
Halikadhalika Mhe. Ulega amefafanua kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kukomesha uvuvi haramu katika maji ya asili iwe baharini au katika maziwa ili kuhakikisha unapungua na kukomeshwa kabisa
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Taasisi ya AU-IBAR, Dkt. Mohamed Seisay amesema kuwa kongamano hilo la siku tatu kuanzia tarehe 16-18 linahusu kujadili Sera, Sheria na Kanuni za Uvuvi za Kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) akifungua kongamano la wadau la kujadili Sera, Sheria na Kanuni za Uvuvi za Kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika lililofanyika kwenye Ukumbi wa Peacock hoteli jijini Dar es salaam Agosti 16,2023.
Sehemu ya wadau wa kongamano la kujadili Sera, Sheria na kanuni za Uvuvi za Kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika Agosti 16, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kulia) akiongea na waandishi wa habari mda mfupi mara baada ya kufungua kongamano la wadau la kujadili Sera, Sheria na Kanuni za Uvuvi za Kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika Agosti 16, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau wa Uvuvi mara baada ya kufungua Kongamano la kujadili Sera, Sheria na Kanuni za Uvuvi za Kimataifa ili ziweze kutumika katika mabadiliko ya mfumo wa Sekta za Uvuvi Barani Afrika lililofanyika kwenye ukumbi wa peacock hotel jijini Dar es Salaam, Agosti 16,2023.