Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wamejizatiti kuhakikisha Tanzania inakuwa mzalishaji mkubwa wa chakula kwa ajili ya matumizi ya ndani na nje ya nchi.
Ameyasema hayo leo Agosti 22 jijini hapa alipokuwa akifungua warsha ya siku tatu ya wahariri na waandishi wa habari, ikiwa ni maandalizi ya Jukwaa la Mifumo ya Chakula (AGRF) linalotarajiwa kufanyika Septemba.
"Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwani tayari tumeanza na BBT LIFE (Building a Better Tomorrow- Livestock and fisheries Enterpreneurs), ili tuwe na uzalishaji mkubwa.
"Tuna vijana 700 wanaofundishwa kule Tanga, Mwanza na Kagera," alisema.
"Sasa kuna fedha za mabadiliko ya tabia nchi, ambazo mkulima anaweza kulima majani ya mifugo ambayo yatasaidie kuondoa hewa ukaa na kufanya biashara.
"Tunaitaka bandari ije haraka ili tusafirishe mifugo, tutasafirishe mbuzi, maana wengine wanataka wachinje wenyewe. Sio tunavutana tu, tunataka mambo yatokee haraka," amesisitiza.
Kuhusu masoko, amesema yatapatikana kwani uzalishaji unaendelea kuongezeka.
"Tumenunua ndege inayoweza kubeba tani 60, ambazo ni sawa na kiwanda kimoja tu cha samaki pale Mwanza.
"Katika msimu wa 2021, tuliuza tani 1,724; Mwaka 2022/ 23 tumeuza tani 14,000, kwa hiyo tunaomba ushirikiano wenu," amesema.
Kuhusu AGRF, Waziri Ulega amesema awali sekta za mifugo na uvuvi hazikuwepo, lakini katika mkutano uliofanyika Kigali nchini Rwanda, sekta hizo ziliingizwa.
"Kwa mara ya kwanza mkutano huu unafanyika nchini ukiwa na mifugo na uvuvi.
Ujio wa mkutano huo ni fursa adhimu, tunataka tuilishe dunia kupitia kilimo. Kauli mbiu yetu ni 'vijana na wanawake ndio kiini cha uzalishaji."
Kwa upande wake Meneja Mkazi wa Taasisi ya Kilimo ya Afrika (Aggra), Vianey Rweyendela amesema Tanzania imepata fursa kubwa kwankuwa na mkutano wa AGRF.
"Huu ni wakati wetu kuitangaza nchi yetu. kwa sasa tunaelekea kukuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
"Hakuna nchi iliyokwepa umasikini lakini kupitia kilimo tunaweza kujikwamua. Kwa uchambuzi tumeufanya, tumesema tusipotenga Sh5 trilioni kwenye wizara zinazohusika na kilimo, hatutatoka kwenye umasikini," amesema.
Naye mwakilishi wa taasisi ya Utafiti wa Mifugo (ILRI), Dk James Rao amesema elimu zaidi inahitajika kuelewa umuhimu wa mifugo kwa lishe na uchumi.
"Miaka michache iliyopita mifugo ilipewa jina baya la kuharibu mazingira, wakisema inazalisha hewa ukaa, lakini ukweli ni kwamba inachangia kuboresha mazingira na hili linapaswa kuelezwa," amesema.
"Mifugo inachangia asilimia 40 katika mazao ya kilimo na sehemu nyingine hadi asilimia 80. Inachangia kuboresha lishe, ajira na malighafi za bidhaa.
Mbali na wataalamu na waandishi wa habari, mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salim Mtambile.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akiongea wakati akifungua mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea mkutano wa AGRF utakaoanza Septemba 5 hadi 8, 2023. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
Kaimu Katibu Mkuu, Dkt. Daniel Mushi akitoa neno la utangulizi kabla ya ufunguzi wa mafunzo kwa Wahariri na Waandishi wa Habari kuelekea mkutano wa AGRF. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wahariri na Waandishi wa Habari muda mfupi baada ya kufungua Mafunzo kwa wahariri hao kuelekea mkutano wa AGRF. Mafunzo hayo ya siku 3 yameanza jijini Dar es Salaam leo Agosti 22 hadi 24, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni