Nav bar

Alhamisi, 31 Agosti 2023

WALIOCHOCHEA MGOGORO WA WAKULIMA NA WAFUGAJI LINDI KUKIONA

◾ Silinde na Sagini wacharuka! 


Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini wameamuru kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria wale wote waliohusika kwenye mauaji yaliyotokana na mgogoro wa wafugaji na wakulima kwenye kijiji cha Ngunichile wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.


Viongozi hao wamebainisha hayo leo Agosti 30, 2023 muda mfupi baada ya kufika kijijini hapo kwa ajili ya kuona hali halisi ya mgogoro huo ambapo wamevitaka vyombo vya usalama kuwakamata watuhumiwa wote wa mauaji yaliyotokana na mgogoro huo na kuwafikisha mahakamani.


"Wakulima na wafugaji wote ni Watanzania na ni wajibu wetu kama viongozi na watendaji kuhakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi na ndio maana Mhe. Rais Dkt. Samia ametuamini na kutuweka katika nafasi tulizonazo" Ameongeza Mhe. Silinde.


Aidha Mhe. Silinde amebainisha kuwa uchunguzi wake umebaini migogoro hiyo inachochewa na baadhi ya Viongozi wasio waaminifu kutoka ngazi za kata na vijiji ambao mara nyingi wamekuwa wakiwaruhusu wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye maeneo wasiyoruhusiwa.


"Katika kuhakikisha tunakomesha kabisa migogoro ya aina hii Septemba Mosi mwaka huu uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi na sekretarieti yake yote utakutana na wakuu wa Mikoa yote ya Kusini na ile ya Pwani ili kujadili taarifa ya kikosi kazi tulichokiunda na hatimaye tutoke na maazimio ya pamoja yatakayotekelezwa na pande zote" Ameongeza Mhe. Silinde.


Kwa upande wake Naibu Waziri wa mambo ya ndani Mhe. Jumanne Sagini amewataka wananchi wa kijiji hicho waliokuwa wamekimbia makazi yao kwa kuhofia hali ya usalama warejee na kufanya shughuli zao kama kawaida.


"Serikali ya Dkt. Samia kamwe haiwezi kuacha watu wakimbie makazi yao kwa kuhofia usalama wao na kama hali hiyo itaendelea maana yake hata sisi aliotuamini kulinda raia na mali zake hatutoshi kwenye nafasi zetu" Amesema Mhe. Sagini.


Mhe. Sagini amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa kijiji hicho kulinda amani wakati wote na kuwa vinara wa kutoa taarifa pale wanapohisi jambo lolote linaloashiria uvunjaji wa amani.


Hivi Karibuni kumeibuka migogoro baina ya wafugaji na wakulima mkoani Lindi huku chanzo kikubwa cha migogoro hiyo kikiwa ni uvamizi unaofanywa na wafugaji kwenye baadhi ya maeneo ya wakulima.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) akimueleza jambo Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani Mhe. Jumanne Sagini kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Agosti 30, 2023 muda mfupi kabla ya kuelekea kwenye kijiji cha Ngunichile kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kulia) akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe. Mohammed Moyo muda mfupi baada ya kuwasili wilayani hapo Agosti 30, 2023 kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji kwenye kijiji cha Ngunichile.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi Agosti 30, 2023 alikofika kwa lengo la kutafuta suluhu ya mgogoro wa wakulima na wafugaji wilayani Nachingwea.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni