Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi na ile ya China kupitia Wizara ya Sayansi na Teknolojia zimekubaliana kuimarisha sekta ya Uvuvi kwa kushirikiana katika kuongeza teknolojia ya utekelezaji wa shughuli za uvuvi nchini.
Makubaliano hayo baina ya nchi hizo mbili yamefanywa jijini Wuhan nchini China Julai 06, 2023 na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde huku upande wa China ukiwakilishwa na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa nchi hiyo Mhe. Zhang Guangjun.
"Serikali yetu inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kabisa kuhakikisha sekta hii ya Uvuvi inakuwa na mchango mkubwa katika
kuondokana na changamoto ya ajira kwa vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za vyuo mbalimbali kule nchini kwetu lakini pia iwe na mchango mkubwa kwenye pato la Taifa " Amesema Mhe. Silinde.
Mhe. Silinde ameongeza kuwa Wizara yake inaamini ushirikiano huo utaongeza chachu ya ubunifu kwenye miundombinu ya kusindika mazao ya uvuvi jambo ambalo litaongeza ubora wa mazao hayo na hivyo kuongeza kiwango cha mazao yanayouzwa soko la ndani na nje ya nchi.
Akibainisha maeneo ya kipaumbele kwenye ushirikiano huo, Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa China Mhe. Zhang Guangjun amesema kuwa eneo la kwanza litakuwa ni mafunzo kwa wataalam wa uvuvi na eneo la utafiti na ubunifu katika kuendeleza uvuvi wa kisasa.
Ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde nchini China inalenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na China kwa upande wa Sekta za Mifugo na Uvuvi.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa China Mhe. Zhang Guangjun wakikabidhiana nyaraka zinazobainisha maeneo ya ushirikiano baina ya pande hizo jijini Wuhan Julai 06, 2023.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. David Silinde (kushoto) na Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa China Mhe. Zhang Guangjun wakisaini nyaraka zinazobainisha maeneo ya ushirikiano baina ya pande hizo jijini Wuhan Julai 06, 2023.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni