Nav bar

Ijumaa, 19 Mei 2023

​SERIKALI YAJA NA MPANGO ENDELEVU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI

 SERIKALI YAJA NA MPANGO ENDELEVU WA UNYWAJI MAZIWA SHULENI 


 

Na. Edward Kondela

 


Serikali iko kwenye mkakati wa kukamilisha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, ili kuhakikisha wanafunzi wanakunywa maziwa ili kuimarisha afya zao.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe, amebainisha hayo leo (11.05.2023) mara baada ya kufungua rasmi kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, kilichofanyika jijini Dodoma.


Prof. Shemdoe amesema kumekuwa na changamoto ya unywaji maziwa nchini kutokana na takwimu za Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ambapo mtu mmoja kwa mwaka anatakiwa kunywa wastani wa lita 200 ila kwa sasa mtu mmoja kwa mwaka anakunywa lita 62 pekee.


“Kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambao ndiyo wazalishaii  wa maziwa kwenye mnyororo wa thamani tunaanza sisi huko kwenye mifugo tumeona ni vyema kwa kushirikiana wadau wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) na FAO kuhakikisha watoto shuleni wanapata maziwa.” Amesema Prof. Shemdoe


Ameongeza kuwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali mpango kazi huo utaielekeza serikali na sekta binafsi namna ya kuutekeleza katika kuchangia upatikanaji wa maziwa shuleni ili kuongeza idadi ya shule ambazo zimekuwa zikipata maziwa kupitia mpango huo.


Kwa upande wake Mkuu wa Lishe kutoka UNICEF – Tanzania, Bw. Patrick Codjia amesema huu ni mpango mzuri wa wizara katika kuweka msisitizo wa kuimarisha lishe hususan kwa wanafunzi ili kuimarisha afya zao kupitia unywaji maziwa pamoja na kuhamasisha wanafunzi kunywa au kula vitu ambavyo ni muhimu kwao afya zao.


Bw. Codjia amebainisha kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeonyesha nia na jitihada madhubuti katika kuhahikisha inaboresha afya ya watoto kwa kupata lishe bora kupitia unywaji wa maziwa.


Naye Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Dkt. George Msalya amefafanua kuwa mpango wa unywaji maziwa shuleni umekuwa ukitekelezwa hapa nchini kwenye shule mbalimbali ambapo kuna wakati ulifika shule 113 na kufikia wanafunzi Elfu 90.


Aidha amesema mpango kazi huo ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Tarehe 1 Mwezi Juni Mwaka 2023 kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Duniani ambapo utawezesha watekelezaji wa mpango kuona namna nzuri ya utekelezaji wa unywaji maziwa shuleni kwa kushirikiana na UNICEF ambapo Bodi ya Maziwa iliwashirikisha wadau mbalimbali kuandika mpango huo.


Nao baadhi ya washiriki wa kikao hicho wamesema mpango wa unywaji maziwa shuleni ni muhimu katika kuimarisha afya za watoto na kuleta chachu kwa wasindikaji wa maziwa kuwa na vifungashio vya bei nafuu ambavyo mzazi anaweza kumudu kwa ajili ya kumnunulia mwanaye maziwa.


Kikao cha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni kilichofanyika jijini Dodoma kimeshirikisha wizara za kisekta, taasisi za serikali, vyuo vikuu, wadau kutoka sekta binafsi, wazalishaji wa maziwa, wasindikaji wa maziwa, shule zinazotekeleza mpango wa unywaji maziwa, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo.

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe akizungumza jijini Dodoma wakati akifungua rasmi kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni, ambapo amesema serikali iko kwenye mkakati wa kukamilisha mpango huo ili kuhakikisha wanafunzi wanakunywa maziwa na kuimarisha afya zao. (11.05.2023)

Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Stephen Michael akizungumzia juu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni na namna serikali ilivyopitia hatua mbalimbali katika kuuandaa, wakati wa kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango huo kwenye kikao kilichofanyika jijini Dodoma. (11.05.2023)

Msajili wa Bodi ya Maziwa nchini Dkt. George Msalya akifafanua kwa washiriki juu ya mpango wa unywaji maziwa shuleni katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma, ikiwa ni mapitio ya mwisho kabla ya mpango huo kuzinduliwa rasmi Tarehe 1 Mwezi Juni Mwaka 2023 kwenye siku ya kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Maziwa Duniani. (11.05.2023)

Mkuu wa Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa Linalohudumia Watoto (UNICEF) – Tanzania, Bw. Patrick Codjia akifafanua juu ya umuhimu wa lishe bora kwa watoto wakati wa kikao cha mapitio ya mwisho ya mpango wa unywaji maziwa shuleni. Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma. (11.05.2023)

Washiriki wa kikao cha mpango kazi wa unywaji maziwa shuleni kilichofanyika jijini Dodoma kutoka wizara za kisekta, taasisi za serikali, vyuo vikuu, wadau kutoka sekta binafsi, wazalishaji wa maziwa, wasindikaji wa maziwa, shule zinazotekeleza mpango wa unywaji maziwa, taasisi za kifedha na wadau wa maendeleo. (11.05.2023)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni