Nav bar

Jumamosi, 6 Mei 2023

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA 2023/2024

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha bajeti ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.


Bajeti hiyo iliyowasilishwa Mei 2, 2023 na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega ilikuwa na jumla Shilingi Bilioni 292.5, ambapo sekta ya Mifugo fungu 99 ni Shilingi Bilioni 112.1 na Sekta ya Uvuvi fungu 64 ni Shilingi Bilioni 180.5, na Bunge baada ya kuijadili liliridhia kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na matumizi mengine ya kawaida.

 

Katika bajeti hiyo iliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, upande wa mifugo ulikuwa na vipaumbe ambavyo ni kuongeza malisho ya mifugo, kuongeza soko la Biashara ya Nyama, kuchochea ufugaji wa kisasa, kuongeza fursa za ajira na kipato kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Mifugo na kuongeza mchango wa ufugaji kwenye pato la taifa.

 

Kwenye upande wa Sekta ya Uvuvi fungu 64, vipaumbele vililivyowasilishwa ni kusudio la kuanzisha Mamlaka ya Uvuvi, kuwawezesha wavuvi kupata boti za kuvua kwenye kina kirefu, kutoa mikopo isiyo na riba kwa wavuvi wadogo, kuongeza ufugaji wa samaki ili kukidhi mahitaji, kuongeza fursa za ajira na kipato kwenye mnyororo wa thamani wa Sekta ya Uvuvi na kuongeza mchango wa Uvuvi kwenye pato la taifa.

 

Wakati akihitimisha kujibu hoja zilizoibuliwa na wabunge, Waziri Ulega aliwasihi wabunge kuendelea kuipa wizara ushirikiano katika kuhakikisha yale yote yaliyopangwa kutekelezwa kwenye bajeti hiyo iliyopitishwa yanakwenda kutimizwa kwa wakati.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni