Nav bar

Alhamisi, 23 Machi 2023

SERIKALI KUKOPESHA WANAWAKE SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

Serikali kupitia Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (EIB) inatarajia kutoa mkopo wa Sh1.3 trilioni kusaidia wanawake kuboresha biashara na uwekezaji kwenye mnyororo wa thamani katika sekta za mifugo na uvuvi.

Akizungumza kuhusu fursa hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya mifugo na uvuvi Dkt. Daniel Mushi alisema dhumuni la fedha hiyo ni kuwezesha sekta binafsi kuwa kichocheo cha maendeleo, Machi 21, 2023

“Kwa kuanzia walengwa mahsusi ni sekta binafsi hususan kwa biashara zinazoongozwa na wanawake au shughuli zinazoambatana na uchumi wa buluu ikiwemo kilimo cha mwani”alisema Dkt. Mushi.

Aidha Dkt. Mushi alisema sio tu kuwainua wanawake katika uwekezaji bali hata kuzalisha fursa za ajira kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya bahari na mifugo kwa ujumla na kupunguza suala la ukosefu wa ajira nchini.

“Wajasiriamali watumie fursa hii vizuri ili iwe kioo na baadae tuaminike ili fedha zijazo zipitie moja kwa moja kwenye sekta binafsi na fursa hii itakuja tena ikiwa tutakuwa waaminifu kwa kutumia vizuri mikopo hiyo”alisema.

Akizungumza katika mkutano wa kuwajengea uwezo na kujadili fursa za mkopo huo, Mchumi kutoka Wizara ya fedha na Mipango Vidah Malle alisema mkopo huo ni fursa pekee kwa sekta binafsi kukuza uaminifu kwa kutoa matokeo chanya ya fedha watakazozichukua.

“Sina uhakika kama fursa kama hii imewahi kupitia katika sekta binafsi mara nyingi hupitia Taasisi za Serikali kwa hiyo hii ni hatua nzuri na tumeoneshwa kuaminiwa hivyo tujitahidi tutakapopata fedha hizo basi tulete matokeo chanya”alisema Vidah.

Kaimu Mkuu kitengo cha kilimo rejareja NMB, Wogofya Mfalamagole alisema benki yao imejipanga kutoa mikopo hiyo kwa wawekezaji wote kwenye sekta binafsi kwa mujibu wa taratibu walizopangiwa na Serikali kwa riba isiyozidi asilimia 10.

Rose Lyimo ni mwekezaji na Katibu wa Chama cha usindikaji wa maziwa Tanzania (TAMPA) alisema katika jamii kuna wanawake wengi wanaofanya shughuli za uwekezaji na hawana mitaji ya kutosha kupanua biashara hivyo mitaji hiyo itasaidia kuwainua wanawake na kuonyesha uwezo wao

Mkopo huo ambao unatajwa kuwalenga zaidi wanawake utakwenda moja kwa moja kwa sekta binafsi kupitia Benki za NMB, CRDB na KCB

 


Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Daniel Mushi akiongea wakati wa kufungua kikao cha wadau juu ya uwezeshwaji wa miradi ya uwekezaji kwenye Mifugo na Uvuvi kupitia dirisha la Uwezeshwaji wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kilichofanyika Machi 21, 2023 Jijini Dodoma

Mchumi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Vidah Malle akiongea wakati wa  kikao cha wadau juu ya uwezeshwaji wa miradi ya uwekezaji kwenye Mifugo na Uvuvi kupitia dirisha la Uwezeshwaji wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kilichofanyika Machi 21, 2023 Jijini Dodoma

Sehemu ya washiriki wa kikao cha wadau juu ya uwezeshwaji wa miradi ya uwekezaji kwenye Mifugo na Uvuvi kupitia dirisha la Uwezeshwaji wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kilichofanyika Machi 21, 2023 Jijini Dodoma


Naibu Katibu Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Dkt. Daniel Mushi (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na wadau mara baada ya kufungua kikao cha wadau juu ya uwezeshwaji wa miradi ya uwekezaji kwenye Mifugo na Uvuvi kupitia dirisha la Uwezeshwaji wa Benki ya Uwekezaji ya Ulaya kilichofanyika Machi 21, 2023 Jijini Dodoma


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni