Na Mbaraka Kambona, Morogoro
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wafugaji nchini kuachana na fikra za kuwa na makundi makubwa ya mifugo ambayo mingi inaishia kufa kwa ukame, na badala yake wawe na utaratibu wa kuivuna na kuiuza ili kuimarisha kipato chao na kuepukana na hasara zinazoweza kuzuilika.
Ndaki alitoa wito huo wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa machinjio ya kisasa ya Nguru Hills iliyofanyika Wilayani Mvomero, mkoani Morogoro Disemba 12, 2022.
“Nitoe wito kwa wafugaji kuanza kufuga kibiashara kwa kuivuna mifugo yao na kuuza kwenye viwanda kama hiki cha Nguru hills. Sambamba na hilo, niwasihi makundi mbalimbali ikiwemo vijana kuchangamkia fursa hii kwa kufanya unenepeshaji wa mifugo na kuwauzia wenye viwanda,” alisema Ndaki
Alisema kuwa uwepo wa viwanda vya kuchakata nyama unaongeza wigo mpana wa soko la mifugo hivyo wafugaji watumie fursa hiyo kwa kuzalisha mifugo yenye tija na kuuza katika viwanda hivyo.
Aliongeza kwa kusema kuwa kwa sasa viwanda vilivyopo nchini vinafanya kazi chini ya uwezo wake uliosimikwa kwa sababu ya ukosefu wa malighafi, kwani pamoja na Tanzania kuwa na mifugo mingi lakini mingi haikidhi vigezo vya kwenda kuchakatwa katika viwanda hivyo.
Waziri Ndaki alisema kuwa machinjio hiyo ya Nguru Hills inatarajiwa kuchinja ng’ombe 100 kila siku, hivyo itatoa fursa kubwa kwa wafugaji ambao watakuwa na mifugo inayokidhi vigezo kuuza katika machinjio hiyo na kujiongezea kipato.
“Wafugaji tubadilike, mazingira mazuri ya ufugaji yanawekwa vizuri na Serikali yenu, chini ya Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tutumie fursa hiyo kuboresha mifugo yetu na tuanze kufuga kibiashara,”aliongeza
Alisema kuwa Wizara yake imeanza kutekeleza mpango wa mabadiliko ya sekta ya mifugo kwa nia ya kuwa na mifugo itakayoweza kuwa malighafi katika viwanda hivyo, na tayari wameanzisha vituo atamizi kwa vijana, ambapo vijana watapewa mtaji wa ng’ombe kumi (10) na kupata mafunzo ya ufugaji bora wa kibiashara kupitia vituo hivyo kwa muda wa mwaka mmoja na baadae wanapisha vijana wengine.
Alifafanua kuwa lengo la Wizara ni kutumia vijana hao kubadili aina ya ufugaji kutoka kwenye ufugaji wa kienyeji kwenda kwenye ufugaji wa kibiashara mpango ambao unakwenda kuwahakikishia wawekezaji kama Nguru hills ukakika wa upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda walivyowekeza.
Waziri Ndaki alisema kuwa miradi mikubwa ya uwekezaji kama ya Nguru Hills ni ukombozi kwa wafugaji na kuwataka wawekezaji kuwa inapotokea jambo lolote lenye nia ya kukwamisha maendeleo ya mradi hasa linalohusu wizara yake wasisite kuwasiliana na Uongozi wa wizara ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa ili mradi uendelee kutoa manufaa yanayotarajiwa.
Meneja Mkuu wa Machinjio ya. Nguru Hills, Bw. Eric Cormark (katikati) akitoa maelezo kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(kushoto) kuhusu mchakato wa uhifadhi wa nyama unavyofanyika katika Machinjio ya Nguru Hills yaliyopo Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro Disemba 12, 2022.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na washiriki wa hafla ya uzinduzi wa Mradi wa Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills uliofanyika Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro Disemba 12, 2022. Machinjio hiyo inatarajiwa kuchinja Ng'ombe 100 kila siku.
Meneja Mkuu wa Machinjio ya Nguru Hills, Bw. Eric Cormark akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki ( wa tatu kutoka kulia) namna mashine zilizopo katika machinjio hiyo zinavyofanyakazi muda mfupi kabla ya kuzindua rasmi Machinjio hiyo Disemba 12, 2022. Wa pili kushoto ni Msajili wa Bodi ya Nyama, Dkt. Daniel Mushi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki(wa pili kutoka kulia) akiangalia namna Ng'ombe anavyochunwa ngozi kwa kutumia mashine ya kisasa muda mfupi kabla ya kuzinduaMradi wa Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills yaliyopo Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro Disemba 12, 2022. Wa tatu kutoka kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Fatma Mwasa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akizindua rasmi mradi wa Machinjio ya Nguru Hills iliyopo Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro Disemba 12, 2022. Wa kwanza kushoto ni Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Dkt. Aggrey Mlimuka.
Meneja Mkuu wa Machinjio ya Nguru Hills, Bw. Eric Cormark akimuonesha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki sehemu ya eneo la Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills iliyopo Wilayani Mvomero, Mkoani Morogoro Disemba 12, 2022. Wengine katika picha ni Viongozi mbalimba kutoka Serikalini na Sekta Binafsi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni