Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo amewataka wazalishaji wa vifaranga vya kuku hapa nchini kuzalishaji vifaranga hivyo kwa kuzingatia ubora wa kitaifa na kimataifa na mahitaji yaliyopo.
Nzunda ameyasema hayo leo (12.12.2022) wakati akifungua kikao
cha Wadau wa Tasnia ya Kuku kilichofanyika kwenye ukumbi wa Hotel ya Royal
Village Jijini Dodoma, kikao ambacho kilijadili hali ya upatikanaji na bei ya
vifaranga na vyakula vya kuku pamoja na kushuka kwa soko na bei ya kuku wa
nyama hapa nchini.
Wazalishaji wa vifaranga vya kuku wametakiwa kujipanga vizuri
ili kuhakikisha wanazalisha vifaranga vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya soko
la ndani ya nchi na kuanza kuangalia uwezekano wa kuuza vifaranga
wanavyozalisha kwenye masoko ya nje ya nchi.
“Anzeni sasa kuzalisha vifaranga vya kuku kuliangalia na
mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, na ili muweze kulifanya hilo ni
lazima mhakikishe vifaranga mnavyozalisha vina kuwa na ubora wa Kitaifa na
kimataifa,” alisema
Katika kikao hicho majadiliano ya kina yalifanyika kuhusu
wajibu wa wazalishaji wa vifaranga, serikali na wadau kwenye mnyororo wa
thamani katika kuzingatia ubora, viwango na katika kuhakikisha kunakuwepo na
uzalishaji wenye tija.
Pia kikao hicho kilijadili namna ya kupunguza gharama za
uzalishaji wa kuku hasa wa nyama kama msingi mmoja wapo wa kuwawezesha wafugaji
wadogo na walaji kumudu gharama. Vilevile wadau wamejadili kuhusu gharama kubwa
za utengenezaji wa chakula cha kuku ili kuona ni namna ya kuweza kuzipunguza na
hivyo kumsaidia mfugaji kupunguza gharama za ufugaji.
Nzunda alisema kuwa Wizara inaendesha vikao hivyo kwa
kuwashirikisha wadau kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya
kuku na kwa kufanya hivyo Wizara inatekeleza mpango wa mabadiliko wa Sekta ya
Mifugo wenye lengo la kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta, kuongeza
uzalishaji na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa.
Aidha, Nzunda amewasisitiza wazalishaji hao kupitia kampuni
zao kuwa na mpango mkakati wa mawasiliano wa kampuni ambao utawasaidia katika
kuwasiliana na wadau wao kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakati. Vilevile kampuni
hizo zimeshauriwa kuwa na mkataba wa huduma kwa mteja katika kuhakikisha huduma
zinatolewa kwa wakati.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron
Nonga amesema kuwa katika kukabiliana na tatizo la soko wadau wameshauri kuwepo
na minada na machinjio ya kuku ambayo itasaidia katika eneo la soko kwa kuwa
kuku watauzwa mnadani lakini pia watachinjwa katika machinjio bora, hivyo
kutakuwa na usalama wa nyama na kuku wataweza kuhifadhiwa vizuri.
Pia Prof. Nonga amewahamasisha wananchi kutumia nyama ya kuku
kwa wingi kwa kuwa ni nyama salama kiafya na kwa kuwa kuku ambao wanafugwa hapa
nchini hawana tatizo lolote kutokana na ubora wa chakula wanachotumia. Aidha,
amewahakikishia wadau hao kuwa serikali inaendelea kudhibiti uingizwaji wa kuku
hapa nchini usiofuata taratibu na kudhibiti magonjwa.
Tariq Machibya ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr. Kuku
Farmers amesema kuwa wafugaji wa kuku wanatakiwa kupatiwa elimu juu ya namna
kifaranga anavyopatikana na utaratibu wa upataji wa vifaranga. Hii itawasaidia wafugaji kwa kutoa oda kwa
wakati na wazalishaji kuzalisha vifaranga kwa wakati na hivyo kuondoa
malalamiko yanayotolewa kutokana na kukosekana kwa vifaranga. Hivyo ameshauri
njia mbalimbali za utoaji elimu zitumike na wazalishaji wa vifaranga pamoja na
serikali ikiwemo ya matumizi ya mitandao ya kijamii.
Pia amewashauri wazalishaji wengine kuanza kulima nafaka
ambazo zinatumika katika kutengenezea chakula cha kuku ili kupunguza gharama. Vilevile
amewasihi vijana kuona na kutumia fursa ya uwekezaji kupitia tasnia ya kuku,
kwa kuwa bidhaa hiyo inatumika kila siku hivyo soko lake ni la uhakika.
Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku, Manase Mrindwa ameishukuru
serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna ambavyo imekuwa
ikishirikiana na wadau hao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Aidha, ameiomba wizara kuendelea kuwasaidia wadau hao kupitia vyama vyao ili
tasnia ya kuku iweze kuwa imara hapa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni