Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia Sekta ya Uvuvi imefanya kikao kazi kwa ajili ya kuandaa nyaraka zitakazosaidia kuimarisha utendaji kazi wa Dawati la Jinsia la sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha
Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi, Bi. Meresia Mparazo wakati akifungua kikao
hicho kilichofanyika kwenye hotel ya Kings Way mkoani Morogoro.
Sekta ya Uvuvi imeanzisha Dawati la Jinsia ili liweze kushughulikia
masuala yote yanayohusu sekta ya uvuvi katika muktadha wa jinsia yanashughulikiwa
katika uendelezaji, uimarishaji na usimamizi wa rasilimali za uvuvi.
Bi. Mparazo amesema kuwa dawati hilo limeanzishwa ili kutatua
changamoto za jinsia kwa wanaume na wanawake wanaojishughulisha na shughuli za
uvuvi. Kupitia dawati hilo wameweza kuanzisha Jukwaa la Wanawake Tanzania
wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi (TAWFA).
Mratibu wa Dawati la Jinsia kutoka Sekta ya Uvuvi, Bi. Upendo
Hamidu amesema kuwa watu waliochangia kuanzishwa kwa Dawati la Jinsia ni Jukwaa
la Wanawake Tanzania wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi (TAWFA) pamoja na
wanaume na wanawake wanaojishughulisha na Uvuvi.
Upendo amesema lengo la dawati kutatua changamoto zinazowagusa
wanawake na wanaume katika shughuli za uvuvi na sio wanawake peke yake katika
masuala ya kijinsia japo kwa takwimu za sasa wanawake wanachangamoto nyingi
zaidi.
Hivyo uwepo wa dawati hili utakuwa mkombozi kwa wadau kwa
kuwa dawati litakwenda kutatua changamoto za kijinsia zinazowakabili ili kila
mmoja anayejishughulisha na uvuvi aweze kunufaika na rasilimali hizo.
Naye Lilian Ibengwe ambaye ni Afisa Uvuvi Mwandamizi amesema
kuwa kupitia kikao kazi hicho, mipango ya kuimarisha dawati inakwenda
kuandaliwa, hivyo wadau wanaojishughulisha na uvuvi watambue kuwa serikali
inafuatilia masuala ya jinsia katika Sekta ya Uvuvi.
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi, Bi. Meresia Mparazo (katikati waliokaa) akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki wa warsha ya kuandaa nyaraka za dawati la jinsia la sekta ya uvuvi iliyofanyika mkoani Morogoro mara baada ya kufungua warsha hiyo. (14.11.2022)
Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi, Bi. Meresia Mparazo akifungua warsha ya kuandaa nyaraka za dawati la jinsia la sekta ya uvuvi iliyofanyika mkoani Morogoro. (14.11.2022)
Baadhi ya washiriki wa warsha ya kuandaa nyaraka za dawati la jinsia la sekta ya uvuvi wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa. (14.11.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni