Na. Elieda Euzebius
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka Maafisa Ugani wote nchini kuhakikisha wanajisajili katika mfumo ya M- Kilimo ili waweze kuwafikia wafugaji wengi zaidi na kutatua changamoto mbalimbali wanazo kumbana nazo.
Mhe. Ndaki aliyasema hayo wakati akifungua Mafunzo Rejea kwa Maafisa Ugani wa Kata na Vijiji kwa Mikoa ya kanda ya kati ya Dodoma na Singida yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya chamwino, Dodoma Novemba 14, 2022.
Alisema kuwa mpaka sasa jumla ya Maafisa Ugani 3,018 kati ya 3,201 ndiyo wamesajiliwa katika Mfumo wa M- Kilimo huku akiwahimiza maafisa ugani ambao bado hawajajisajili wafanye hivyo haraka.
“Vilevile, niwahimize kuwahamasisha wafugaji katika maeneo yenu kuweza kujisajili katika Mfumo wa M-Kilimo ili tuweze kufikia lengo la kusajili wafugaji 1,000,000 nchini ifikapo Juni, 2023”, alisema Mhe. Ndaki
Halikadhalika, Waziri Ndaki alisema kuwa Wizara imeanza matumizi ya mifumo ya TEHAMA (Ugani Kiganjani) kwa lengo la kuwafikia wafugaji wengi na kutoa mrejesho wa kila kazi ambayo Afisa Ugani atakuwa ametekeleza katika eneo lake.
Aliongeza kwa kusema katika kutatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vya kutolea huduma za Ugani, Wizara imepanga kununua pikipiki 1,200 na magari 13 ambayo yatagawiwa katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Bw. Tixon Nzunda alisema Serikali imejipanga kufanya mabadiliko katika sekta ya mifugo na kuainisha maeneo kadhaa kama dira ya utekelezaji wa mabadiliko hayo.Baadhi ya vipaumbele alivyovitaja ni pamoja na kuboresha upatikanaji wa uhakika wa malisho na maji, ufugaji wenye tija, kuanzisha mashamba darasa ya malisho, kubadilisha Ranchi za Taifa pamoja na kuimarisha masoko na minada.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Gift Msuya aliiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuongeza Wataalam wa mifugo na vitendea kazi vya kutosha kulingana na mifugo iliyomo wilayani Chamwino kwani Wilaya hiyo Asilimia 60 ya pato lake linatokana na shughuli za sekta ya mifugo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni