Katibu Mkuu anayesimamia Sekta ya Mifugo, Bw. Tixon Nzunda amewataka wasimamizi wa Vituo Atamizi vya Ufugaji Mifugo Kibiashara kwa Vijana kuwa wabunifu na kuhakikisha wanasimami utekelezaji wa mwongozo uliotolewa kuhusu vituo hivyo.
Nzunda ameyasema hayo leo (21.09.2022)
wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya wasimamizi wa vituo atamizi vya
ufugaji mifugo kibiashara kwa vijana yaliyofanyika kwenye Chuo cha Mafunzo ya
Mifugo Kampasi ya Morogoro.
Wasimamizi hao wa vituo
wametakiwa kuwa wabunifu hasa katika kukabiliana na changamoto watakazo kutana
nazo, huku wakitakiwa kuwajenga vijana hao uwezo wa kuweza kufuga kisasa kwa
vitendo, kuwa na mahusiano na mawasiliano mazuri ambayo yatawasaidia katika
masoko ya mifugo pamoja na mazao ya mifugo watakayokuwa wanazalisha.
Lakini pia amewataka wasimamizi
hao kuwapatia vijana elimu ya utunzaji wa malisho na upandaji wa malisho mapya
ili hata watakapotoka katika vituo hivyo waweze kwenda kuanzisha mashamba ya
malisho kwa ajili ya mifugo yao.
Nzunda amesema serikali kwa
sasa imeamua kufungua milango kwa vijana kupitia Sekta ya Mifugo ambapo vituo
hivyo vitasaidia kuwabadilisha vijana kifikra kuhusu ufugaji, kupunguza tatizo
la ajira, na kuongeza uzalishaji wa mifugo na mazao yake kwa kuzingatia viwango
na kuongeza kipato cha vijana na taifa kwa ujumla.
Serikali katika kuhakikisha
vituo hivi vinaanza kazi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imatenga kiasi cha
shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuanza kupata mafunzo ya
ufugaji wa kisasa kwenye vituo 8 vilivyopo LITA na TALIRI ambapo usahili wa vijana
hao tayari ulishakamilika.
“Vijana hawa wanakwenda
kupatiwa ujuzi kuhusu maisha, ujuzi kuhusu uzalishaji wa kazi, ujuzi wa
uzalishaji fedha, ujuzi wa kupata mitaji, na ujuzi wa kwenda kujenga uchumi wa nchi
kupitia Sekta ya Mifugo,” alisema Katibu Mkuu Nzunda
Vijana waliochaguliwa
kujiunga na vituo atamizi wametakiwa kuwa na moyo wa kujituma na kujitambua
kwamba wao ni wawekezaji ambao wameingia kuwekeza kwenye Sekta ya Mifugo.
Nzunda ameitaka LITA na
TALIRI kuhakikisha kazi hii inaanza kutekelezwa Septemba 26, 2022 na kwamba
fedha zilizotolewa kwa kazi hii zisitumike kwa ajili ya kuendeshea ofisi wala
kazi nyingine yoyote nje ya kazi iliyokusudiwa na serikali.
Mtendaji
Mkuu wa Wakala ya Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA), Dkt. Pius
Mwambene amesema kuwa LITA inakwenda kuanzisha vituo 6 katika kampasi za
Kikulula (Kagera), Mabuki (Mwanza) na Buhuri (Tanga) ambapo kila kituo kitachukua
vijana 30 ambao watafundishwa namna ya kufuga kibiashara kwa muda wa miezi 12.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya wasimamizi wa Vituo Atamizi vya Ufugaji Mifugo Kibiashara kwa Vijana yaliyofanyika kwenye Chuo cha Mafunzo ya Mifugo Kampasi ya Morogoro wakifuatilia mada zilizokuwa zinawasilishwa wakati wa mafunzo hayo. (21.09.2022)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Tixon Nzunda akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Shamba katika Chama cha Ushirika cha Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUGECO), Marcelina Lubuva (kushoto) wakati alipokuwa akikagua shamba la alizeti kwenye kituo chao. (21.09.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni