Nav bar

Alhamisi, 22 Septemba 2022

SERIKALI ITATOA ZAIDI YA SHILINGI BIL. 30.9 KWA WAVUVI-NDAKI

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki ameweka wazi hatua ambazo Serikali imechukua ili kuendelea kuboresha sekta ya Uvuvi nchini ikiwa ni pamoja na kutenga mkopo usio na riba wa zaidi ya shilingi   bilioni 30.9 ambao utatolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo kwa vikundi vya wavuvi ili waweze kununua boti za kisasa za uvuvi na kutengeneza miundombinu bora itakayowawezesha kufuga samaki kwenye vizimba.


Mhe. Ndaki ameyasema hayo leo (21.09.2022) wakati akifungua Mkutano uliolenga kujadili utekelezaji wa Mpango kabambe wa miaka 15 wa sekta ya Uvuvi uliofanyika kwenye Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar-es-Salaam ambapo mbali na kuwashukuru wadau mbalimbali wa Maendeleo walioshiriki kutengeneza mpango huo ametoa rai kwa wadau hao kuendelea kuiunga mkono Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika kufanikisha utekelezaji wa mpango huo.


“Mbali na mkopo huo, Serikali pia imeendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kujenga na kuboresha  mialo, masoko na vituo mbalimbali vya kuzalishia vifaranga vya samaki na kuboresha biashara ya mazao ya uvuvi ndani nan je ya nchi.


Aidha Mhe. Ndaki amebainisha kuwa kwa muda mrefu sekta ya Uvuvi imekuwa mkombozi wa kiuchumi hasa kwa kundi la vijana na wanawake ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa ndio watekelezaji wakubwa wa shughuli hizo jambo ambalo limeendelea kuihamasisha Serikali kuwajengea mazingira wezeshi ya kufanya Shughuli zao.


Mpango Kabambe wa miaka 15 wa Sekta ya Uvuvi ulizinduliwa jana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo wakati wa utekelezaji wake unatarajiwa kuwa suluhu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wavuvi hapa nchini.

Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Bw. Magese Bulayi akiwasilisha taarifa ya Maendeleo ya sekta ya Uvuvi wakati wa Mkutano wa kujadili Mpango Kabambe wa miaka 15 wa sekta ya Uvuvi uliofanyika leo (21.09.2022) kwenye Ukumbi wa Maktaba-Chuo kikuu cha Dar-es-salaam.

Sehemu ya wadau wa sekta ya Uvuvi nchini wakifuatilia taarifa ya Maendeleo ya Sekta ya Uvuvi iliyokuwa ikitolewa na Mkurugenzi wa Uvuvi nchini Bw. Magese Bulayi (hayupo pichani) wakati wa Mkutano wa kujadili Mpango Kabambe wa miaka 15 wa sekta ya Uvuvi uliofanyika leo (21.09.2022) kwenye Ukumbi wa Maktaba-Chuo kikuu cha Dar-es-salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni