Na. Edward Kondela
Serikali imesema Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga kinawekewa mipango maalum ya kuwa shamba darasa la uchumi wa mifugo ambapo kwa kuanzia itaweka kambi hivi karibuni kwa ajili ya kuhamasisha upandishaji wa mbegu bora za ng’ombe wa kisasa.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo (02.07.2022) alipotembelea na kujionea miundombinu inayokarabatiwa na kujengwa kwa ajili ya shughuli za mifugo hususan katika maeneo ambayo wakazi waliohamia katika maeneo ya kijiji hicho kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro iliyopo Mkoani Arusha, ambapo amesema nia ya serikali ni kutaka shughuli za ufugaji katika kijiji hicho iwe bora na kisasa zaidi.
Naibu Waziri Ulega amesema kambi hiyo inatarajia kupandisha mbegu bora za ng’ombe wa kisasa zaidi ya elfu nne ili hatimaye Kijiji cha Msomera hapo baadae kiwe na ng’ombe wengi wa kisasa na bora ambao watatoa maziwa mengi ya kutosha pamoja na nyama.
Amesema kuwa tayari serikali imetenga zaidi ya Shilingi Milioni 160 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha ukusanyaji maziwa katika Kijiji cha Msomera kutokana na idadi ya mifugo inayozidi kuhamia katika maeneo ya kijiji hicho inayomilikiwa na wakazi waliohamia kutoka Hifadhi ya Ngorongoro ikiwa ni moja ya njia ya kuvutia wawekezaji juu ya uwepo wa maziwa mengi kijijini hapo pamoja na kuvutia ujenzi wa viwanda vya kuchakata maziwa.
“Msomera itakuwa eneo maalum kwa uchumi wa mifugo, miundombinu inaendelea kujengwa, leo nimeshuhudia majosho yakikarabatiwa na nimeshuhudia ng’ombe zaidi ya elfu moja wa wakazi wa Kijiji cha Msomera wakiogeshwa pia kuna kazi kubwa inaendelea ya kujengwa bwawa la kuhifadhia maji kwa ajili ya mifugo na binadamu.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha, ameongeza kuwa serikali inaendelea kutenga bajeti ili kuwepo na kliniki ya mifugo pamoja na mnada wa mifugo wa kisasa ili Kijiji cha Msomera kiwe shamba darasa kote nchini kwa uchumi wa mifugo na watu kujifunza kupitia kijiji hicho na kuvutia watu zaidi hususan wakazi wanaohamia kutoka katika Hifadhi ya Ngorongoro kufanya ufugaji wa kisasa na kibiashara zaidi.
Kwa upande kwake Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchemba amesema mikakati iliyopo ni kutoa elimu kwa wafugaji wote katika Kijiji cha Msomera ambapo tayari serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeanza mazungumzo juu ya namna ya utoaji wa elimu bora ya ufugaji wa kisasa.
Mhe. Mchemba amesema ndani ya muda mfupi tayari hali ya kiafya ya mifugo mbalimbali hususan ng’ombe imeanza kubadilika kutokana na uwepo wa malisho mengi pamoja na maji hivyo kuanza kuongeza uzalishaji wa maziwa ya kutosha.
Mkuu huyo wa wilaya amebainisha kuwa wakazi ambao bado wapo katika Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha ambao wanahamasishwa kuhamia katika Kijiji cha Msomera kilichopo Mkoani Tanga kwa ajili ya kuboresha maisha yao kwa kupata huduma za msingi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuwa serikali inazidi kuweka mikakati mbalimbali ili Kijiji cha Msomera kuwa cha mfano katika ufugaji wa kisasa.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kijiji cha Msomera, mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Martin Oleikayo Paraketi ameishuru serikali kwa namna inavyozidi kuboresha miundombinu ya wafugaji ambapo Wizara ya Mifugo na Uvuvi tayari inasimamia uwepo wa maji na malisho kwa ajili ya wafugaji.
Bw. Paraketi anasema wamefurahishwa sana na ujenzi wa bwawa kubwa la kuhifadhia maji kwa ajili ya mifugo na binadamu, linalojengwa na serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni Mbili na litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya lita milioni saba.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega, amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ili kujionea ukarabati na ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya wafugaji yakiwemo majosho ya kuogeshea mifugo, bwawa la kuhifadhia maji kwa ajili ya mifugo na binadamu pamoja na maeneo ya malisho ya mifugo.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyenyanyua ndoo ya maji) akishiriki katika ujenzi wa moja ya miundombinu kwa ajili ya shughuli za ufugaji katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika kijiji hicho na kuhamasisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikamilike katika muda uliopangwa au ikiwezekana mapema zaidi. (02.07.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (aliyenyanyua fimbo) akitoa maelezo kwa viongozi wa Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kujionea ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya shughuli za ufugaji yakiwemo majosho ya kuogeshea mifugo. Pembeni yake kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchemba. (02.07.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (wa pili kutoka kulia) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mhe. Siriel Mchemba (kushoto kwake), wakati Naibu Waziri Ulega alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera na kupata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho waliohamia kutoka Hifadhi ya Ngorongoro Mkoani Arusha na kukagua mabirika ya kunyweshea mifugo maji. (02.07.2022)
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega akisoma kibao kinachoainisha eneo maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo na kukagua eneo hilo wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga. (02.07.2022)
Picha ya muonekano wa maendeleo ya ujenzi wa bwawa la kuhifadhia maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo na binadamu kwa wakazi wa Kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga. Bwawa hilo litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita zaidi ya milioni saba na linajengwa na serikali kwa gharama ya Shilingi Bilioni Mbili. (02.07.2022)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni