Nav bar

Jumatatu, 18 Julai 2022

KIWANGO CHA UUZAJI WA NYAMA NJE YA NCHI CHAONGEZEKA

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema kuwa Tanzania imeongeza kiwango cha uuzaji wa nyama inayosindikwa hapa nchini nje ya nchi kutoka Tani 1700 zilizosafirishwa kwa kipindi cha miezi 6 ya kwanza mwaka jana hadi tani 10,000 zilizosafirishwa kwa kipindi cha Mwezi Januari hadi Juni mwaka huu.

Mhe. Ndaki ameyasema hayo muda mfupi baada ya kufungua mkutano unaolenga kufanya tathmini ya mnyororo wa thamani wa nyama nyekundu na wanyama hai kwa upande wa nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi (ECOWAS) unaofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 04-08, 2022.
“Kwa hiyo utaona soko letu limeongezeka sana na katika kuboresha mnyororo wa thamani wa nyama nyekundu kupitia mradi huu wa Umoja wa Afrika Tanzania tumenufaika na mambo mawili, la kwanza ni uboreshwaji wa mifugo yetu hasa maeneo ya Longido na Loliondo ambapo tumeweza kutumia aina ya ng’ombe wanaoitwa ‘Sahiwal’ na kupitia mradi unaitwa ‘Pare White goat’ unaotekelezwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha ambao pia unatusaidia sana kuboresha mbuzi wetu wa nyama na maziwa” Amesema Mhe. Ndaki.
Katika kuhakikisha utaalam huo wa uboreshaji wa mifugo unaenea nchi nzima, Mhe. Ndaki amebainisha kuwa tayari amezungumza na wasimamizi wa mradi huo kutoka Shirika linalounganisha nchi za Afrika kwa upande wa rasilimali za wanyama (AU-IBAR) ili wasambaze mbegu hizo za ng’ombe na mbuzi katika maeneo yote nchini ambapo amewataka kuanza na maeneo yanayojishughulisha na ufugaji kwa kiasi kikubwa.
Akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Shirika linalounganisha nchi za Afrika kwa upande wa rasilimali za wanyama (AU-IBAR) Dkt. Nick Nwankpa amesema kuwa ajenda ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2063 na mpango mkakati wa Shirika hilo wa mwaka 2018-2023 vyote kwa pamoja vinatambua rasilimali za wanyama ndio msingi mkuu unaosaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi wengi barani Afrika.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo nchini Prof. Hezron Nonga (wa kwanza) na baadhi ya watendaji wa Sekta ya Mifugo wakiandika baadhi ya dondoo kwenye Mkutano wa tathmini ya mnyororo wa thamani wa nyama nyekundu na wanyama hai kwa upande wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi (ECOWAS) unaofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 4-8, 2022.

Kaimu Mkurugenzi kutoka Shirika linalounganisha nchi za Afrika kwa upande wa Rasilimali za Wanyama (AU-IBAR) Dkt. Nick Nwankpa (kulia) akimkabidhi Zawadi Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki muda mfupi baada ya Mhe. Ndaki kufungua Mkutano unaolenga kufanya tathmini ya mnyororo wa thamani wa nyama nyekundu na wanyama hai kwa upande wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi (ECOWAS) unaofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 4-8, 2022.


Daktari wa Mifugo kutoka Kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (NAIC) Dkt. Dafay Buay akiandika dondoo kwenye Mkutano wa tathmini ya mnyororo wa thamani wa nyama nyekundu na wanyama hai kwa upande wa nchi za Jumuiya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi (ECOWAS) unaofanyika jijini Arusha kuanzia Julai 4-8, 2022.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni