Nav bar

Jumatatu, 9 Mei 2022

SEKTA YA UVUVI ENDELEVU NA KISASA KIUCHUMI YATAJWA KUFIKIA 2025

Na. Edward Kondela


Serikali imesema utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26 ulioanza hivi karibuni unalenga kuifanya Sekta ya Uvuvi na ukuzaji viumbe maji kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele katika mpango huo.


Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Rashid Tamatamah amebainisha hayo (04.04.2022) Mjini Morogoro katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wakati akifungua warsha ya wadau wa Sekta ya Uvuvi, kutathmini mafanikio na mikakati ya kukuza mazao ya uvuvi nchini ambapo ameeleza kuwa mpango huo unaolenga kukidhi matarajio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ukiwa na lengo la kuboresha hali ya maisha ya watanzania.


Dkt. Tamatamah ameongeza kuwa ili kufanikisha azma hiyo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inayo dhamira ya kuwa na Sekta ya Uvuvi endelevu na kisasa kiuchumi, kijamii na mazingira kufikia Mwaka 2025, ambapo ametaja kuwa serikali imedhamiria kufanya mambo mbalimbali yakiwemo ya kuwezesha ununuzi wa meli na ujenzi wa bandari ya uvuvi hususan Shirika la Uvuvi Tanzania (TAFICO), kuwezesha sekta binafsi kuanzisha na kukarabati viwanda vya mazao ya uvuvi, kuhifadhi na kulinda maeneo tengefu ya bahari na maji baridi, kulinda na kuhifadhi makazi ya viumbe muhimu na viumbe wa majini walio katika hatari ya kutoweka.


“Kuwezesha na kuhamasisha uwekezaji katika miundombinu ya uvuvi, vifaa na ufugaji wa kibiashara wa samaki, kuwezesha upatikanaji wa mitaji, utalaamu, ujuzi, maarifa na zana za kisasa za uvuvi kwa wavuvi wadogo na wanawake kupitia vikundi vya kijamii, kufungamanisha utafiti, ugani, uvuvi na kilimo cha majini, kudhibiti ubora, usalama na viwango vya mazao ya samaki na uvuvi, kuboresha maabara za uhakiki wa ubora wa rasilimali za majini na maeneo ya gati za uvuvi, kuwezesha mipango ya matumizi endelevu na usimamizi wa rasilimali za bahari na kuhamasisha utalii katika maeneo tengefu ya bahari.” Amesema Dkt. Tamatamah


Aidha katibu mkuu huyo amesema licha ya Sekta ya Uvuvi kuwa miongoni mwa sekta za kipaumbele katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/22 – 2025/26, mchango wake katika Pato la Taifa (GDP) bado uko chini ambapo ametolea mfano, Mwaka 2020 Sekta ya Uvuvi ilichangia asilimia 1.71 katika pato la taifa na ukuaji wake kwa mwaka ulikuwa asilimia 6.7 pekee na kutaja kuwa kiwango hicho cha ukuaji bado ni cha chini hasa ikilinganishwa na uwepo wa rasilimali anuai za maji ikiwemo bahari, maziwa makubwa na madogo, mabwawa, mito na ardhi oevu.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael Madalla, akizungumza katika warsha hiyo ya wadau wa Sekta ya Uvuvi, kutathmini mafanikio na mikakati ya kukuza mazao ya uvuvi nchini amesema tasnia ya ukuzaji viumbe maji nchini imekuwa ikiendelea kukua kila mwaka kwa wananchi kuwekeza katika ufugaji samaki.


Pia, Dkt. Madalla amesema ni wakati muhimu sasa kwa wananchi kuendelea kuitikia wito huo wa ufugaji samaki ukizingatia kwa sasa serikali imekuwa ikiendelea kuimarisha vituo vyake vya ukuzaji viumbe maji ili kuhakikisha upatikanaji wa wingi wa vifaranga vya samaki maeneo mbalimbali nchini kwa kujenga vituo vipya.


Kuhusu mazingira bora ya uwekezaji, amebainisha kuwa idara yake inaendelea kuboresha mazingira bora zaidi ya uwekezaji ili wananchi watakaoingia katika tasnia ya ufugaji samaki waweze kufuga kibiashara na ufugaji huo uwe endelevu.


Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Uendelezaji wa Rasilimali za Uvuvi Bi. Merisia Mparazo, akimwakilisha Mkurugenzi wa Idara ya Uvuvi Bw. Emmanuel Bulayi, amebainisha mikakati ya kuendeleza Sekta ya Uvuvi ili kuongeza uzalishaji wa samaki. 


Bi. Mparazo amesema kutokana na ongezeko la samaki katika maji ya asili kumekuwa kukichangia kutoa ajira kwa wingi katika Sekta ya Uvuvi hivyo kuna haja ya kuzidi kuendeleza vipaumbele vyenye viashiria vya kukuza zaidi sekta hiyo ili uwepo wa upatikanaji wa samaki wengi zaidi watakaouzwa ndani na nje ya nchi na kuhakikisha upatikanaji wa ajira.


Bw. Said Meck Sadick ni mmoja wa wadau wakubwa wanaofuga samaki kwa njia ya vizimba katika Ziwa Victoria, ambaye amewaambia wadau waliohudhuria warsha ya kutathmini mafanikio na mikakati ya kukuza mazao ya uvuvi nchini, inayofanyika kwa siku tatu Mjini Morogoro kuwa tasnia ya ufugaji samaki inalipa na kuwasihi watu wanaotaka kufuga samaki kutumia wataalam ili waweze kufuga kwa tija na kupata matokeo mazuri.


Pia amesema ni wakati mzuri kwa wataalam kuwa na muda wa kuwatembelea wafugaji na kuwahamasisha namna ya kufuga kisasa kwa kuwa baadhi ya watu hawajui namna ya kuwapata wataalamu hao na kuwapatia elimu ya ufugaji samaki pamoja na kuwasimamia ili wapate matokeo mazuri.


Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaamini kuwa mchango wa sekta ya uvuvi katika pato la taifa unaweza kupanda zaidi ya asilimia tano, iwapo kutakuwa na usimamizi na uvunaji endelevu wa rasilimali za uvuvi kwenye vyanzo vya asili  pamoja na ukuzaji wa kisasa wa viumbe maji.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni