Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Tixon Nzunda amewataka Wataalam wa Mifugo nchini kutumia taaluma zao kuwasaidia wafugaji kuondokana na changamoto zinazowakabili hususan magonjwa ya mifugo.
Nzunda alitoa wito huo wakati akifunga mafunzo ya ufuatiliaji, utoaji taarifa na ukabilianaji wa magonjwa ya Wanyama kwa wataalamu wa Afya ya Mifugo katika tukio lililofanyika jijini Dar es Salaam Machi 31, 2022.
Wakati akifunga mafunzo hayo, aliwataka wataalam hao kwenda kutumia mafunzo hayo kwa vitendo kwa kusaidia jamii ya wafugaji kwa kuwaelimisha juu ya ufugaji bora na kutoa huduma za ugani zinazostahili kwa wafugaji hao.
“Haitakuwa na maana kama mafunzo haya ya miezi minne mliyoyapata halafu matendo yenu yashindwe kubadilisha maisha ya watu, nendeni mkatumie hayo maarifa kuwasaidia watu”, alisema
Aliongeza kwa kusema kuwa wataalam hao wanapaswa kuyafikisha mafunzo hayo pia kwa watoa maamuzi, wafugaji na watunga sera ili yaweze kutekelezwa na kuleta tija inayotarajiwa kwa jamii.
Aidha, aliwashukuru washirika wa Maendeleo wakiwemo Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID) kwa kuwezesha mafunzo ya kujenga uwezo wataalam hao katika kufuatilia magonjwa ya Wanyama na yale yanayoambukiza binadamu kutoka kwa wanyama.
Alisisitiza kwa kusema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa Sekta ya Mifugo kwa sababu magonjwa ni moja ya kikwazo kikubwa katika uzalishaji wa mifugo, mazao ya mifugo na biashara kwa ujumla huku akisema kuwa takribani asilimia 70 ya magonjwa mapya ya milipuko yanayoambukiza binadamu yanatokana na Wanyama.
Naye Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Dkt. Nyabenyi Tipo alishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata na aliahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazokabili sekta ya mifugo nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni