Nav bar

Jumatatu, 10 Januari 2022

WAVUVI WATAKIWA KUPIGA VITA UVUVI HARAMU*

Na Mbaraka Kambona,

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wavuvi kupinga vitendo vya uvuvi haramu na kutunza Rasilimali za Uvuvi kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.

Waziri Ndaki alitoa wito huo alipokuwa akiongea na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Magarini uliopo katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera Disemba 13, 2021.

Wakati akiongea na wavuvi hao alisema kuwa  uvuvi haramu ni sumu kwa biashara ya Samaki na Dagaa hivyo ni muhimu kuendelea kuutokomeza ili rasilimali za uvuvi ziweze kuwa na tija kwa Taifa.

"Anayefanya uvuvi haramu hatutakii mema sisi na watoto wetu, kwa hiyo huyo ni adui namba moja kwetu sisi sote," alisema

Waziri Ndaki pamoja na kuwapongeza wavuvi hao kwa jitihada wanazozichukua katika kupinga vitendo vya watu wachache wanaofanya uvuvi haramu aliwahimiza kuendelea kupinga vitendo hivyo ili rasilimali hizo ziweze kuleta manufaa kwa Taifa.

Naye, Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah alisema pamoja na shughuli hizo za uvuvi kuendelea kuwapatia kipato wavuvi na Serikali, lengo la Serikali ni kuona rasilimali hizo zinavuliwa kwa uendelevu ili ziweze kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

"Tukivua bila kuzingatia uendelevu, hii rasilimali ndani ya miaka miwili mitatu itapotea na hata wafanyabiashara wanaokuja kutoka Rwanda hawatakuja tena hapa," alisema Dkt. Tamatamah

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mhe. Toba Nguvila alimueleza Waziri Ndaki kuwa Wilaya hiyo imepiga hatua kubwa katika kupinga uvuvi haramu kwa kushirikiana na wananchi, huku akimuomba Waziri huyo kuwasaidia vifaa ikiwemo Boti ili viweze kuwasaidia katika Doria za kuzuia uvuvi haramu Wilayani humo.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndaki pia alitembelea soko la kuuzia Samaki na Dagaa la Kasenda lililopo katika Wilaya ya Chato, Mkoani Geita ambapo akiwa katika soko hilo aliwahimiza wafanyabiashara hao kuendelea kufanyabiashara kwani Serikali imelijenga soko hilo kimkakati kwa lengo la kupata mapato yatokanayo na mazao ya uvuvi.


Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongea na Wavuvi wanaofanya shughuli zao katika Mwalo wa Magarini uliopo katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera Disemba 13, 2021. 

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akiongea na Wafanyabiashara wa Soko la Kasenda lililopo katika Wilaya ya Chato, Mkoani Geita Disemba 13, 2021. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni