Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ameipa Kampuni ya ZECO yapewa siku 14 kukamilisha ukarabati wab wawa la Kimokuwa litakalotumika kwa ajili ya matumizi ya kunyweshea mifugo na matumizi ya binadamu.
Prof. Gabriel ametoa
maelekezo hayo leo (22.12.2020) wakati alipotembelea kukagua maendeleo ya
ukarabati wa mradi huo unaotekelezwa katika kijiji cha Kimokuwa, wilayani Longido,
mkoani Arusha.
“Mwanzoni kampuni hii ilianza
kazi vizuri lakini mwishoni imekuwa na matatizo kwani usimamizi wao wa mradi
sio mzuri kitu ambacho kimesababisha umaliziaji wa mradi kuwa na mapungufu,”
alisema Prof. Gabriel.
Pia amemtaka mkandarasi
kujiridhisha kwenye kingo za bwawa hilo walizoziweka kwani ikitokea zikabomoka
hatua kali zitachukuliwa dhidi ya kampuni hiyo.
Kutokana na mapungufu
aliyoyaona amempa mkandarasi siku 14 kuhakikisha anakamilisha mradi. Kutokana na
kuwepo kwa mapungufu hayo, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Pauline Gekul
hataupokea mradi huo kama ilivyokuwa imepangwa hapo awali.
Prof. Gabriel amewasihi wakandarasi
wazawa kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa umakini ili waendelee kuheshimika na
kupewa kazi na serikali kwani fedha zinazotolewa za miradi zinatoka kwa
wananchi walipa kodi. Hivyo amewataka wafanye kazi kwa uadilifu na kwa kuzingatia
viwango.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya
ya Longido, Bw. Simba amempogeza Katibu Mkuu Gabriel kwa uamuzi wake wa kukagua
maendeleo ya mradi huo kabla ya kukabidhiwa kwa mapungufu yaliyopo hata uongozi
wa wilaya ulishayabaini. Lakini pia amemsihi mkandarasi kuhakikisha anayafanyia
kazi mapungufu yote yaliyoainishwa katika ukaguzi huo ili wafugaji na jamii kwa
ujumla iweze kupata huduma hiyo ya maji.
Mwenyekiti wa Kijiji cha
Kimokuwa, Bw. Kileli Olendere amesema Katibu Mkuu yupo sahihi kuamua kutomleta
Naibu Waziri kuja kukabidhiwa bwawa hilo kwani ukarabati wake bado
haujakamilika hivyo ni vema mkandarasi kwanza akamilishe kazi zinazotakiwa
ndipo mradi ukabidhiwe kwa viongozi pamoja na wananchi.
Zephania Umbuli ambaye ni Mkurugenzi
wa Kampuni ya ZECO Construction amesema ameyapokea maelekeo yaliyotolewa na
Katibu Mkuu Gabriel na ameahidi kuyatekeleza ndani ya siku 14 walizopewa.
Ukarabati wa bwawa hili la Kimokuwa
unaogharimu milioni 511.9 ulitakiwa kukamilika Novemba 25. 2020 lakini mkandarasi
aliomba kuongezewa muda mpaka Decemba 10. 2020. Kutokana na mapungufu yaliyoainishwa
amepewa siku 14 mpaka Januari 06, 2021 kuhakikisha anakamilisha kazi vinginevyo
hatua za kimkataba zitaanza kuchukuliwa.
Bwawa la Kimokuwa linaloendelea kukarabatiwa na Kampuni ya ZECO Construction kwa ajili ya kunyweshea maji mifugo na matumizi ya binadamu lililopo katika Kijiji cha Kimokuwa, wilaya ya Longido, mkoani Arusha. (22.12.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akionyesha moja ya mapungufu aliyoyabaini wakati wa ukaguzi wa mradi wa ukarabati wa bwawa la Kimokowua lililopo wilayani Longido, mkoani Arusha. (22.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni