Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema Tanzania ina chanjo za kutosha dhidi ya magonjwa ya mifugo na kuagiza wafugaji wote nchini pamoja na maeneo ambayo serikali inafuga kuhakikisha mifugo yao inachanjwa ili kuondokana na magonjwa hayo.
Akizungumza jana (24.12.2020)
mara baada ya kutembelea Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Wilaya ya
Kibaha Mkoani Pwani, wakati wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo, Waziri
Ndaki amesema ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na mifugo bora inayokidhi soko
la kimataifa ni lazima mifugo ichanjwe dhidi ya magonjwa ili yapatikane mazao
bora ya mifugo.
“Tunayo chanjo ya kutosha
hivyo niwatake wafugaji wote ikiwa ni pamoja na sisi serikali kwenye maeneo
ambayo tunafuga tuchanje mifugo yetu ili tupate mifugo iliyo bora, tunataka
sasa nchi yetu iende kwenye ubora badala ya uwingi wa mifugo, ili tupate nyama
bora na maziwa bora kwa maana ya mazao bora ya mifugo ili tuweze kuuza katika
soko la kimataifa.” Amesema Mhe. Ndaki
Katika ziara hiyo kwenye
taasisi ya TVI, Waziri Ndaki alitaka kufahamu namna agizo alilolitoa hivi
karibuni la ng’ombe waliopo kwenye ranchi 14 za taifa kuchanjwa dhidi ya
ugonjwa wa homa ya mapafu kutokana na baadhi ya mifugo hiyo kuathiriwa na
ugonjwa huo katika Ranchi ya Kongwa iliyopo Mkoani Dodoma, ambapo Kaimu
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ambayo
inaisimamia TVI, Dkt. Stella Bitanyi amesema chanjo zimesambazwa kutokana na
mahitaji ya ranchi hizo na sasa wapo katika hatua ya chanjo hizo kuwafikia
majirani wa ranchi hizo ili kuweza kuchanja ng’ombe wao.
Aidha, Waziri Ndaki amejionea
ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha HESTER kilichopo Wilayani Kibaha na
kupongeza hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa katika ujenzi huo na kusema mara
kiwanda hicho kitakapoanza kufanya kazi Mwezi Aprili Mwaka 2021, kitasaidia
kuongeza wigo wa uwepo wa chanjo nyingi hapa nchini na kusaidia endapo magonjwa
ya mifugo yatajitokeza.
“Hii inaonesha umuhimu wa
kuwa na chanjo tayari kwa ajili ya mifugo yetu yote ili ikitokea magonjwa ya
milipuko tuweze kupata mahali pa kusaidiwa kwa karibu na pengine kwa bei nafuu
kwa kuwa chanjo hizi zitakuwa zinazalishwa hapa nchini.” Amefafanua Mhe. Ndaki
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki amefika pia katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama
cha TAN CHOICE kilichopo Wilayani Kibaha, na kubainisha kuwa umuhimu wa uwepo
wa viwanda hivyo kutasaidia kubadilisha fikra za wafugaji kwa kuingia kwenye
ufugaji bora.
Kuhusu changamoto ya vibali
vya kuingiza nyama zilizochakatwa kwenye baadhi ya nchi kutoka Tanzania, Waziri
Ndaki amesema wizara itawasiliana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa pamoja na Wizara ya Viwanda na Biashara ili kufahamu changamoto
zinazovikabili baadhi ya viwanda kushindwa kusafirisha nyama kwenda baadhi ya
nchi kutokana na kukosa vibali vya kuingiza nyama hizo kutoka Tanzania.
Pia, amefafanua kuwa uwepo wa
viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama nchini kunazidi kusaidia kukuza
biashara ya mifugo nchini na kuongeza wigo wa soko la mifugo hivyo ni muhimu
kwa wafugaji kuanza kuhakikisha wanakuwa na mifugo iliyo bora ili waweze kuuza
mifugo yao kwa bei nzuri na waweze kunufaika kiuchumi na taifa pia liweze
kupata mapato ya kutosha kupitia biashara ya mifugo.
Awali akiwa katika Ofisi ya
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekutana
na mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo ambapo wamezungumza mambo
mbalimbali yanayohusu sekta za mifugo na uvuvi.
Katika mazungumzo hayo
Mhandisi Ndikilo amesema kwa sasa migogoro ya wakulima na wafugaji imepungua
kwa kiasi kikubwa huku akitaka juhudi zaidi zifanyike katika kuwapatia wafugaji
elimu ya kuwa na mifugo michache na yenye tija badala ya kuwa na mifugo mingi
ambayo haitoshi kutokana na uwepo wa maeneo ya kufugia.
Kwa upande wake Waziri Ndaki
amesema changamoto zinazohusu wizara atahakikisha zinafanyiwa kazi ili sekta za
mifugo na uvuvi ziwe endelevu na kuondokana na migogoro isiyo na tija kwa
taifa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amemaliza ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Pwani, ambapo katika siku ya kwanza (23.12.2020) alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wafugaji Wilayani Rufiji na kuwataka kuheshimu maeneo waliyopewa na uongozi wa mkoa kwa ajili ya ufugaji na kuacha kuingia katika maeneo ya wakulima.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto) akiangalia namna nyama ya mbuzi
ilivyohifadhiwa katika chumba chenye baridi kali kabla ya taratibu nyingine za
kusafirisha nyama hiyo kwenda nje ya nchi. Waziri Ndaki amefanya ziara ya
kikazi ya siku moja katika kiwanda cha kuchinja na kuchakata nyama TAN CHOICE kilichopo
Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani. (24.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa pili kulia) akishuhudia namna kiwanda cha kuchinja na
kuchakata nyama TAN CHOICE kinavyofanya kazi wakati alipofanya ziara ya kikazi
katika kiwanda hicho kilichopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani na kuwataka
wafugaji waanze kubadilisha fikra zao na kufuga kisasa kwa kuwa viwanda vya
namna hiyo vinahitaji nyama bora ili kukidhi soko la kimataifa. (24.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki akishuhudia namna wataalam wa Taasisi ya Chanjo Tanzania
(TVI), wakiwa kwenye moja ya hatua za kuzalisha chanjo dhidi ya magonjwa ya
mifugo ambapo Waziri Ndaki ameridhishwa na utendaji kazi wa taasisi hiyo na
kusisitiza kuwa chanjo zinazozalishwa katika kituo hicho zinatosheleza mahitaji
ya nchi na kuwataka wafugaji kuchanja mifugo yao. (24.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza) akikagua mitambo mbalimbali iliyofungwa katika
kiwanda cha kuzalisha chanjo HESTER ambacho kinajengwa Wilayani Kibaha, Mkoani
Pwani, ambapo Waziri Ndaki amesema uwepo wa viwanda vingi vya chanjo hapa
nchini kutasaidia nchi kuwa tayari kukabiliana na magonjwa yoyote ya mifugo
pindi mlipuko wa magonjwa ukitokea. (24.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi
Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kulia) akishuhudia chanjo mbalimbali
zinazozalishwa na Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyo chini ya Wakala ya
Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), wakati alipofanya ziara ya kikazi ya
siku moja katika taasisi hiyo iliyopo Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani ili
kushuhudia chanjo zinazozalishwa hapa nchini. (24.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni