Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali
itaandaa mfumo shirikishi na endelevu wa kudhibiti zaidi uvuvi haramu ambao
utafanya mikoa na wilaya zishiriki kikamilifu katika kutokomeza uvuvi huo
badala ya kuwa na operesheni za kutafuta wavuvi haramu.
Waziri Ndaki amebainisha hayo (21.12.2020) alipokuwa katika
mkutano wa hadhara na wakazi wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili, kilichopo
Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo na
kubainisha kuwa mfumo huo utasaidia serikali kuondokana na operesheni za za
vipindi maalum na badala yake mfumo uwe unafanya kazi siku zote.
“Tuwe na mfumo endelevu wa kumaliza kabisa tatizo la uvuvi
haramu kwa hiyo tutafanya hivyo badala ya kuwa na operesheni au zimamoto ya
kutafuta wavuvi haramu tuwe na mfumo unaofanya kazi siku zote huku mikoani,
wilayani na mahali pengine popote.” Amesema Mhe. Ndaki
Waziri Ndaki amewataka pia watu wanaojihusisha na wanaofikiria
kujiingiza katika uvuvi haramu kwamba watatafutwa popote watakapokuwa na
watapata adhabu kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni za nchi huku
akipongeza wananchi wanaoishi Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kwa kudhibiti
uvuvi haramu hususan unaotumia mabomu ambao kwa mujibu wa taarifa ya Mkoa wa
Lindi, uvuvi huo umedhibitiwa kwa asilimia mia moja, huku akiahidi kuyafanyia
kazi mapungufu yaliyopo ndani ya wizara katika kudhibiti uvuvi
haramu.
Aidha, kuhusu zao la mwani Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki akizungumza na wakazi hao wa Kijiji cha Mchinga Namba Mbili
ameyataka makampuni yanayonunua zao hilo kutumia mizani zilizo sahihi na kuacha
mara moja kuwadhulumu wakulima hao na kuwataka pia wakulima kuangalia uwezekano
wa kuliongezea thamani zao hilo ili kuuza kwa bei nzuri tofauti na bei ya sasa
ya kilo moja kwa Shilingi Elfu Moja ambayo wakulima hao wanasema
haitoshelezi.
Pia, amesema wizara itaangalia utaratibu kwa kushirikiana na
halmashauri kuwawezesha wakulima wa mwani kupitia vikundi vyao katika
kutengeneza bidhaa zitokanazo na mwani badala ya kuuza kama malighafi ili
waweze kunufaika zaidi kibiashara kwa kujiongezea mapato.
Awali akiwa katika Ofisi za Mkoa wa Lindi, Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesomewa taarifa ya mkoa huo na Mkuu wa Wilaya ya
Lindi Bw. Shaibu Ndemanga ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa huo Bw. Godfrey
Zambi ambapo taarifa hiyo imebainisha mkoa kwa kushirikina na wizara umedhibiti
uvuvi haramu kwa asilimia mia moja na kubainisha kuwa mkoa utaendelea
kuhakikisha unadhibiti kabisa vitendo hivyo.
“Mheshimiwa Waziri katika eneo hili tumefanya vizuri sana miaka
mitano iliyopita tusingeweza kusafiri kutoka pale Mnazi mmoja hadi hapa mkoani
bila kusikia bomu tuna zaidi ya miaka mitatu hadi minne hatujasikia bomu kwa
hili tumedhibiti kwa asilimia mia moja.” Amesema Bw. Ndemanga
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Lindi, Mbunge wa
Jimbo la Mchinga Mama Salma Kikwete amemwambia Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe.
Mashimba Ndaki wavuvi wa mkoa huo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya vifaa
vya uvuvi kwa kuwa wanatumia zana duni badala ya kutumia boti za kisasa na
kuwepo kwa soko la kisasa la kuuzia mazao ya samaki, huku akitaka pia akinamama
wawezeshwe katika kilimo cha mwani hususan suala la bei.
“Lindi tuna changamoto za vitendea kazi tunakuomba mheshimiwa
waziri ulichukue suala la changamoto uende nalo ukalifanyie kazi ninaamini na
ninajua baada ya muda mfupi tutapata majibu ambayo ni chanya hususan katika
upatikanaji wa boti ya kisasa ya uvuvi na suala la bei ya zao la mwani.”
Amefafanua Mama Kikwete.
Mapema akiwa njiani kuelekea Mkoani Lindi kuanza ziara ya kikazi
ya siku mbili mkoani humo, ikiwa ya kwanza kikazi nje ya Mkoa wa Dodoma tangu
kuapishwa kushika wadhifa huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. John Magufuli, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amefika
katika ofisi za taasisi na wakala zilizo chini ya wizara hiyo zilizopo Kata ya
Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani na kuwataka watumishi hususan wa Kituo
cha Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi (FRP) kufuata sheria, taratibu
na kanuni zilizopo katika kudhibiti uvuvi haramu na kutowaonea watu kwa
kuwabambikizia kesi.
Amewataka watumishi hao kuwa waaminifu kwa kuhakikisha faini
zinazolipwa ziwe halali za kieletroniki badala ya kuwaandikia faini kwa risiti
za mkono na kutowaonea wavuvi kwa namna yoyote.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki yuko katika ziara
ya kikazi ya siku mbili Mkoani Lindi ambapo anatarajia pia kukutana na wakulima
na wafugaji katika kuhakikisha serikali inaondoa kero za kutoelewana kati ya
watu wanaojishulisha katika sekta hizo mbili.
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza katika mkutano wa hadhara na wakazi wa
Kijiji cha Mchinga Namba Mbili, kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi wakati
wa ziara yake ya kikazi mkoani humo na kubainisha kuwa wizara itaandaa mfumo
shirikishi wa kupambana na uvuvi haramu siku zote badala ya kuwa na operesheni
za vipindi maalum. (21.12.2020)
Mkuu wa Wilaya ya
Lindi Bw. Shaibu Ndemanga ambaye amemwakilisha mkuu wa mkoa wa Lindi Bw.
Godfrey Zambi katika ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki,
akitoa taarifa ya mkoa na namna walivyofanikiwa kutokomeza uvuvi haramu wa
kutumia mabomu kwa asilimia mia moja. (21.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki
(aliyekaa katikati) amepata fursa ya kusikiliza maoni, maswali na kero
mbalimbali za wavuvi alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji cha Mchinga namba
Mbili kilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi na kuahidi kero zinazohusu
wizara atahakikisha anazifanyia kazi ili wavuvi waweze kufanya shughuli zao
bila bughudha na kuwatahadharisha wasijiingize katika uvuvi haramu.
(21.12.2020)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (kulia) akishika zao la mwani wakati alipotembelea mashamba ya zao hilo yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, katika kijiji cha Mchinga Namba Moja mara baada ya kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Mchinga Namba Mbili, vilivyopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi na kuwataka wakulima wa zao hilo waliongezee thamani kwa kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni. (21.12.2020)
Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa ameshika jongoo bahari ambapo ni moja ya mazao
yaliyopo baharini ambayo yana soko kubwa nje ya nchi wakati alipokuwa
anatembelea mashamba ya zao la mwani yaliyopo kwenye Bahari ya Hindi, katika
kijiji cha Mchinga Namba Moja kiilichopo Wilaya ya Mchinga Mkoani Lindi.
(21.12.2020)
Mkurugenzi wa
Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Nazael
Madalla akifafanua namna wizara inavyochukua hatua mbalimbali kuhamasisha
wananchi kufuga samaki, upatikanaji wa vifaranga bora pamoja na vyakula bora
vya samaki, wakati wa kikao cha uongozi wa Mkoa wa Lindi na Waziri wa Mifugo na
Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki aliyefika mkoani hapo kwa ziara ya kikazi ya siku
mbili. (21.12.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni