Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kutekeleza Waraka wa mwaka 2002 ambao unawataka kutenga asilimia 15 ya mapato yanayotokana na shughuli za Sekta ya Mifugo na Uvuvi na kuzirejesha kwenye sekta hizo ili kuboresha shughuli zake.
Gekul alitoa agizo hilo
alipokuwa akiongea na Viongozi wa Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro
alipotembelea kukagua shughuli za Sekta ya mifugo na uvuvi zinazotekelezwa
Wilayani humo Disemba 23, 2020.
Kwa mujibu wa Gekul, mwaka
2002 Serikali ilitoa waraka ambao unaelekeza kuwa Halmashauri zote nchini
zihakikishe kuwa mapato yanayopatikana kutokana na shughuli za sekta ya mifugo
na uvuvi itengwe asilimia 15 na zirudishwe kwa sekta hizo ili kuboresha huduma
kwa mifugo ikiwemo ukarabati wa majosho, minada na kununua chanjo za mifugo.
“Wakurugenzi rejeeni huo
waraka ambao unadumu mpaka mwaka 2025 ili mtekeleze kama ulivyoagiza na
tukifanya hivyo itasaidia kuboresha huduma za mifugo yetu na tupate mazao bora yanayotokana
na mifugo hiyo,” alisema Gekul
Aliendelea kusema kuwa
miundombinu mingi ya kuhudumia mifugo imechoka akitolea mfano minada ya kuuzia
ng’ombe kuwa mingi haina uzio, mifugo inauzwa katika maeneo ya wazi jambo
ambalo linachangia upotevu wa mapato ya Halmashauri.
“Najua katika Halmashauri
zetu mara nyingi fedha huwa hazitoshi lakini ni muhimu kujenga nidhamu ya
matumizi ya fedha na tukifanya hivyo itakuwa rahisi kutenga hizo pesa ili
kuboresha sekta za mifugo na uvuvi, hivyo naagiza baada ya kutoka hapa
tukatekeleze hilo,” alisisitiza Gekul
Aidha, Waziri Gekul alisema
kuwa muelekeo wa serikali kwa sasa ni kuhakikisha majosho yanaboreshwa, minada
inakarabatiwa na chanjo zinapatikana kwa urahisi ili wananchi wasihangaike
kupata huduma kwa ajili ya mifugo yao.
Pia, aliwataka maafisa mifugo
kuhakikisha wanasimamia vyema ukusanyaji wa maduhuli ya serikali ili kuzuia
upotevu wa mapato kwani makusanyo yakiwa mazuri na huduma za mifugo
zitaboreshwa.
Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi (wapili kushoto) akitoa maelezo kwa
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (katikati) kuhusu moja ya nyavu
inayotumiwa na wavuvi wanaofanya shughuli zao katika bwawa la Nyumba ya Mungu
lililopo Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro. Waziri Gekul alikwenda katika
Mwalo wa bwawa hilo kukagua shughuli zinazoendelea hapo Disemba 23, 2020. Wa
kwanza kulia ni Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka.
Wavuvi wa Bwawa la Nyumba ya
Mungu (kushoto) wakimuonesha Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul
(kulia) Samaki aina ya Perege waliovuliwa kutoka katika bwawa hilo muda mfupi
baada ya kumaliza kuongea na wavuvi wanaoishi kandokando mwa bwawa hilo lililopo
Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Disemba 23, 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga,
Thomas Apson akieleza jambo katika mkutano wa Wavuvi wanaofanya shughuli zao
kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline
Gekul (kushoto aliyekaa) uliofanyika
Wilayani Mwanga, Mkoani Kilimanjaro Disemba 23, 2020. Kulia ni
Mkurugenzi, Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni