Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel amesema serikali imelenga kuhakikisha wafugaji nchini wanakuwa na ng’ombe bora, wenye kutoa nyama bora na maziwa mengi wanaopatikana kwa njia ya uhimilishaji (kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya mrija).
Prof. Gabriel amesema hayo
katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wakati akizindua
rasmi kambi ya uhimilishaji katika kijiji hicho kwa wafugaji wa jamii ya
kimasai na kuwataka waache kufuga kwa mazoea bali wawe na ng’ombe bora na wenye
tija huku akiwalenga zaidi akinamama nchini kujikita katika ufugaji wa kisasa.
“Haya ni mafanikio makubwa
niwaombe akinamama wengine Tanzania waige mfano wa kina mama wenzano wa jamii
ya kimasai walioamua kufuga kisasa kwa kuwa na ng’ombe bora hatuwezi kuendelea
kwenye ufugaji wa zamani lazima tufuge kisasa na uhimilishaji unafanyika kwa
ng’ombe yeyote hata wa kienyeji.” Amesema Prof. Gabriel
Prof. Gabriel akizungumzia
faida za uhimilishaji amesema njia hiyo ya kumpatia ng’ombe mimba kwa njia ya
mrija ni muhimu katika kuendeleza ubora wa mifugo hiyo ili kutengenzea mbari na
kosaafu bora ya ng’ombe.
Amefafanua kuwa uhimilishaji
ni muhimu kwa kuwa mfugaji anaweza kuchagua ng’ombe anayemtaka na ubora wake
pamoja na kudhibiti magonjwa ya mifugo hiyo kwa ng’ombe dume kupanda ng’ombe
wengi kwa wakati mmoja.
Ili kutoa hamasa kwa wafugaji
wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali
Mkoani Mbeya Katibu Mkuu Wizara Mifugo na Uvuvi amesema wafugaji
watakaohimilisha ng’ombe elfu moja wa mwanzo wizara itagharamia kama sehemu ya
uzinduzi na uimarishaji wa kambi za uhimilishaji.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo Bw. Stephen Michael
amesema wizara imekuwa ikifanya kazi karibu na wananchi hali iliyofikia kuweka
kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete na kuwafanyia ng’ombe vipimo
kabla ya kupandikizwa mbegu.
Naye Afisa Mifugo kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Fadhil Chamwazi ameongeza kuwa kambi za
uhimilishaji zina malengo ya kuhamasisha wafugaji kutumia huduma ya
uhimilishaji na kuwajengea uwezo jamii ya wafugaji na wataalam juu ya faida ya
uhimilishaji.
Bw. Chamwazi amesema zoezi
hilo limeanza katika mwaka wa fedha 2019/20 na kwa mwaka 2020/2021
limezinduliwa mkoani Tabora na sasa katika Mkoa wa Mbeya katika Kijiji cha
Matebete na kubainisha kuwa vigezo vinavyoangaliwa kwa ng’ombe kabla ya
kupandikizwa mbegu ya uzazi kwa njia ya mrija, wataalamu wanakagua afya ya
ng’ombe pamoja na kuzingatia umri na muonekano wake.
Nao baadhi ya wafugaji wa
jamii ya kimasai katika kijiji hicho wamefurahishwa na zoezi hilo na kuiomba
serikali kuendelea kuwapatia elimu zaidi na kuwafahamisha namna bora zaidi za
ufugaji wa ng’ombe bora wa kisasa ili waweze kupata matokeo chanya katika
ufugaji wao.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akimpongeza mfugaji wa jamii ya
kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya, baada ya
ng’ombe wake kufanyiwa vipimo kwa ajili ya kufanyiwa uhimilishaji. (14.09.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo). Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati), akiwa na
wasichana wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya Mbarali,
Mkoani Mbeya waliohitimu masomo kutoka vyuo mbalimbali nchini. Kutoka kulia ni
Bi. Naishiye Eliakimu amehitimu shahada ya ualimu, Bi. Naumu Silomi amehitimu
diploma ya uhandisi wa ndege, Bi. Rahabu Galahenga amehitimu diploma ya sheria
na Bi. Hawa Julius amehitimu diploma ya ualimu. (14.09.2020)
Kaimu Mkurugenzi wa
Uzalishaji na Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Bw. Stephen
Michael akizungumzia kambi ya uhimilishaji katika Kijiji cha Matebete Wilaya ya
Mbarali, Mkoani Mbeya na namna wizara inayoshirikiana na wananchi ili kuhakikisha
wanapata mifugo bora. (14.09.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyesimama katikati), Kaimu
Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko, Bw. Stephen Michael (aliyesimama upande
wake wa kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji wa Malisho na Rasilimali
za Vyakula vya Mifugo, Dkt. Lovince Asimwe (aliyesimama upande wake wa kushoto)
wakiwa wamevalia mavazi ya kabila la kimasai baada ya kupatiwa zawadi na
wafugaji wa Kijiji cha Matebete. (14.09.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na Bi. Rahabu
Galahenga ambaye amehitimu diploma ya sheria. Prof. Gabriel amefika katika
Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya kwa ajili ya
kuzindua kambi ya uhimilishaji. (14.09.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akizungumza na wafugaji wa jamii
ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya
wakati wa uzinduzi wa kambi ya uhimilishaji katika kijiji hicho. (14.09.2020)
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo
na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (aliyevaa miwani) akiwaongoza
wafugaji wa jamii ya kimasai katika Kijiji cha Matebete kilichopo Wilaya ya
Mbarali Mkoani Mbeya kuzindua zoezi la uhimilishaji (kupandikiza ng’ombe mimba
kwa njia ya mrija). (14.09.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni