Serikali imeagiza kutafutwa kwa watu waliohusika kuwauzia kwa
njia ya mkopo wafugaji ng’ombe wa maziwa waliozaa tayari na kuwahadaa wafugaji
kuwa ng’ombe hao hawana uzao wowote (mitamba) ili wawapatie wafugaji ng’ombe
wenye sifa kama walivyokubaliana katika mikataba.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema hayo
katika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, wakati akikabidhi lori moja la kukusanyia
maziwa lenye uwezo wa kubeba lita 15,000, keni za maziwa 50 pamoja na vifaa vingine vya kuboresha vituo vya
kukusanyia maziwa wilayani humo kwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wafugaji wa
Ng’ombe wa Maziwa Mkoa wa Tanga (TDCU) na kufafanua kuwa serikali imefanya kazi
nzuri kuhakikisha wafugaji wanapata mikopo hiyo kupitia Benki ya Maendeleo ya
Kilimo Tanzania (TADB), hivyo lazima ihakikishe wafugaji hao wananufaika.
“Katika hatua ya upatikanaji wa ng’ombe mkajikuta mkaingia
kwenye mitego ng’ombe ameshakuwa mkongwe halafu huku unaambiwa hana uzao wowote
ilhali ng’ombe amezaa zaidi ya mara mbili, TDCU pamoja na vyama vya msingi
hakikisheni wale waliowazuia ng’ombe wafugaji hawa wanafanya maboresho ili
lengo la serikali liweze kukamilika najua mmeuziana baina yenu lakini hatuwezi
kama serikali kukaa kimya lengo letu ni kuhakikisha mambo yanaenda katika
unyoofu wake.” Amesema Mhe. Ulega
Aidha Mhe. Ulega amefafanua kuwa endapo wafugaji hao wataendelea
kuwa na ng’ombe hao watazidi kuwa masikini kwa kuwa watatumia nguvu kubwa
kuwapatia malisho na dawa za mifugo ilhali ng’ombe hao wanatoa lita chache za
maziwa tofauti na matarajio.
Katika upande mwingine, Naibu Waziri Ulega amewataka pia
wafugaji wa ng’ombe wa maziwa Mkoani Tanga, kuwa waaminifu kwa kuhakikisha
wanapeleka maziwa ya kutosha TDCU ili maziwa hayo yaweze kutosheleza mahitaji
ya kiwanda cha kuchakata maziwa cha Tanga Fresh ambacho kinapokea maziwa
kupitia chama hicho.
Aidha kuhusu bima ya mifugo Naibu Waziri Ulega amefafanua kuwa
Wizara ya Mifugo na Uvuvi imefanya kazi kubwa kwa kushirikiana na Shirika la
Bima la Taifa (NIC) ambapo tayari sera ya bima ya mifugo ipo tayari na kwamba
ipo katika hatua ya mwisho kuzinduliwa mwaka huu ili ianze kutumika na
kuwanufaisha wafugaji pindi wanapopata majanga mbalimbali ya mifugo yao.
Naye Mratibu wa Miradi kutoka shirika la kimataifa la Heifer Bw.
Mark Tsoxo akizungumza juu ya Mradi wa Usindikaji wa Maziwa Tanzania (TMPP)
uliowezesha kupatikana kwa lori la kukusanyia maziwa kwa TDCU lenye thamani ya zaidi ya
Shilingi Milioni 170, amesema mradi huo nchi nzima unafadhili matenki 6 ya kuhifadhi
maziwa yenye ujazo wa lita 24,000, kukarabati vituo 10, jenereta 7, ufadhili
wa malori 5 ya kubebea maziwa pamoja na keni 250.
Bw. Tsoxo amefafanua kuwa kutokana na jitihada za mradi kwa
kushirikiana na wasindikaji, ukusanyaji wa maziwa umeongezeka kwa zaidi ya lita
12,000 kwa siku kutoka kati ya mwezi Januari lita 55,817 kwa siku hadi
sasa lita 68,017 kwa siku.
Nao baadhi ya wafugaji waliopatiwa mikopo ya ng’ombe wa maziwa
pamoja na ujenzi wa mabanda kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB)
wamefurahishwa na hatua hiyo huku wakiomba serikali na taasisi zingine
kuwaboreshea zaidi mazingira ya ufugaji hapa nchini.
Kuhusu elimu juu ya ufugaji bora wa maziwa wafugaji hao
wameiomba Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia wataalam wa wizara hiyo, mikoa na
wilaya kuhakikisha wanawatembelea wafugaji mara kwa mara ili kuwapatia elimu
bora ikiwemo ya kilimo cha malisho bora ya mifugo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni