Nav bar

Alhamisi, 2 Julai 2020

JIJI LA DODOMA LAKABIDHIWA VIFARANGA 650 VYA KUKU

Wizara ya Mifugo na Uvuvi imekabidhi vifaranga 650 vya kuku kwa halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kugawa kwa wafugaji.

Vifaranga hivyo vimekabidhiwa na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Masoko, Dkt. Felix Adam Nandonde leo kwa aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji hilo. Pamoja na vifaranga hivyo pia amekabidhi mifuko 12 ya chakula, dawa, vifaa vya kulishia na kunyweshea maji.

Dkt. Nandonde amesema wizara inamkakati wa kuhamasisha ufugaji wa nyama nyeupe ikiwemo ya kuku. Kuku wamekuwa wakiliwa sana na wananchi na kwa kutambua hilo wizara ikaona ni vyema kuongeza nguvu kwa wafugaji kwa kugawa vifaranga vya kuku.

Wizara imekuwa ikishirikiana na kampuni ya AKM ambayo kazi yake kubwa ni kuhamasisha ufugaji wa kisasa.  Katika kuendeleza hamasa hiyo, wizara imepeleka kuku aina ya kroiler ambao wanakua kwa muda mfupi na kwa uzito unaofikia kilo 2.5 ndani ya miezi miwili.

Dkt. Nandonde amesema kuwa takwimu zinaonyesha tuna kuku milioni 79.1 nchini lakini kati ya hao kuna kuku wa kienyeji wanaokadiriwa kuwa milioni 38.5 na kuku wa kisasa wanakadiriwa kuwa milioni 40.6.

Naye aliyekuwa Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Bw. Davis Mwamfupe ameishukuru wizara ya Mifugo na uvuvi kwa mchango wake katika kuendeleza ufugaji wa kuku hasa kwa vijana. Pia ametoa wito kwa vijana wa maeneo mbalimbali ya jiji la Dodoma kuzitumia fursa za ufugaji hasa wa kuku katika kujinyanyua kiuchumi na kuleta maendeleo katika jamii.

"Tunataka ifike siku hapa na sisi tuwe na kitunda ya Dodoma, aibu iliyoje kuku wanaenda kutafutwa Singida wanapita Dodoma tunawaona kwenye malori wanaenda Dar-es salaam", alisema Mwamfupe.

Mwenyekiti wa kikundi cha ASACRI YOUTH GROUP, Abdallah Chavuma Taratibu ameishukuru wizara kwa mchango huo wa kuku katika kikundi chao ambacho kinafuga kuku, bata na sungura. Vilevile ameahidi kuwa katika kikundi chao watahakikisha wanawatunza kuku hao vizuri.

Baada ya kukabidhi Dr. Nandonde alitembelea kikundi cha ufugaji kuku cha akina mama wa Ipagala (AMI) ambacho kilipata fedha shilingi milioni 50 kutoka Halmashauri ya jiji la Dodoma. Kikundi hicho kilianza ufugaji tarehe 21/01/2020 kikiwa na kuku 100 lakini mpaka sasa kikundi hicho kina kuku 1000.


Mkurugenzi wa idara ya uzalishaji na masoko, Dkt. Felix Nandonde (kushoto) akimkabidhi vifaranga vya kuku aliyekuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Davis Mwamfupe nje ya ofisi ya halmashauri ya Jiji. (02.07.2020).

Mkurugenzi wa idara ya uzalishaji na masoko,  Dkt. Felix Nandonde na Meya wa Jiji la Dodoma, Davis Mwamfupe  wakiwakabidhi vijana wa kikundi cha wafugaji cha ASACRI YOUTH GROUP vifaranga vya kuku. (02.07.2020).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni