Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof.
Elisante Ole Gabriel ameitaka Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo
(LITA) kuwa bunifu ili kuboresha huduma na kuleta tofauti katika shughuli zao
na kufikia malengo yake.
Prof. Ole Gabriel aliyasema hayo alipokuwa akifungua kikao kazi
cha kwanza cha Bodi mpya ya ushauri ya LITA kilichofanyika jijini Dar es Salaam
Julai 25, 2020.
Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Gabriel aliwahimiza
wajumbe wa bodi hiyo kutumia vyema taaluma zao na kuwa wabunifu katika
kuhakikisha LITA inaboresha huduma zake na kuleta mabadiliko chanya ya
kiutendaji ya Wakala hiyo.
"Nawaomba bodi mfanye kazi yenu vizuri na mfanye
maboresho kadri itakavyowezekana, shirikianeni kwa ukaribu na wadau wengine ili
kusaidia kuboresha shughuli zenu," alisema Prof. Gabriel.
Sambamba na hilo, Prof. Gabriel ameitaka bodi hiyo
kuhakikisha inasimamia vyema rasilimali fedha za taasisi hiyo huku akiwaeleza
kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina wakati wote amekuwa mkali na
watu ambao wamekuwa wanatumia vibaya rasilimali za umma.
Aliendelea kueleza kuwa LITA wanaweze kufanikiwa katika
shughuli zao endapo wataweka mikakati ya kuboresha eneo la masoko na habari
ambalo litasaidia kutangaza na kuhamasisha jamii kupitia vyombo vya habari
kutumia huduma zinazotolewa na LITA na kwa njia hiyo wataongeza mapato.
"Hii ni taasisi ya biashara hivyo ni muhimu kuitangaza
vya kutosha ili watu waijue LITA ni nini, ipo wapi na inafanya nini, kwa
kufanya hivyo kutaivuta jamii kutumia huduma zenu," alifafanua Prof.
Gabriel.
"Serikali inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
imefanya kazi kubwa mpaka sasa tumeingia katika uchumi wa kati, hivyo LITA ni
lazima muhakikishe mnaenda sambamba na kasi hii ya uchumi wa kati kwa kuboresha
huduma zenu ikiwemo kubuni vyanzo vingine vya mapato," aliongeza Prof.
Gabriel.
Akiongea mapema katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji
Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt.
Pius Mwambene alisema kuwa mpaka sasa taasisi hiyo imepata mafanikio kadhaa
ikiwemo kuongezeka kwa udahili wa wanafunzi kutoka 798 mwaka 2012/13 hadi
kufikia 3642 mwaka 2019/2020 huku akisema kuwa wameshaongeza Kampasi nyingine
mbili ambazo ni Mabuki, Mwanza na Kikulula, Kagera.
"Kuanzia Mwaka jana tumeanza kutoa gawio katika mfuko
mkuu wa Serikali ambapo tulianza kutoa kiasi cha shilingi milioni 50 mwaka jana
na mwaka huu tumetoa milioni 100,"alifafanua Dkt. Mwambene
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof. Malongo Mlozi alisema
kuwa kufuatia kauli hiyo ya Katibu Mkuu watahakikisha kuwa wataweka utaratibu
kwa kushirikiana na Menejimenti kuangalia mapato na matumizi ya fedha kila
miezi mitatu, huku akieleza kuwa kwa nafasi yao wataendelea kutoa ushauri juu
ya matumizi bora ya rasilimali umma.
Kuhusu suala la ubunifu alisema kuwa wataweka mipango mizuri
kuhakikisha taasisi hiyo kupitia Kampasi zake inajiendesha kibiashara ili
kujiongezea kipato.
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya
Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Bi. Josephine Matiro akipitia Makabrasha
katika kikao cha kwanza cha bodi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (25.07.2020)
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (katikati waliokaa) akiwa
katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Vyuo vya
Mifugo (LITA) muda mfupi baada ya kufungua kikao chao cha kwanza kilichofanyika
jijini Dar es Salaam. Kulia (waliokaa) ni Mwenyekiti wa Bodi ya LITA, Prof.
Malongo Mlozi na Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LlTA, Dkt. Pius
Mwambene. Waliosimama kutoka kulia ni wajumbe wa Bodi hiyo, wa kwanza ni Dkt.
Angello Mwilawa, wa pili ni Bi. Josephine Matiro, katikati ni Prof. Zacharia
Masanyiwa. Kutoka kushoto (wa kwanza) ni Bw. Mark Tsoso na wa pili ni Bi.
Faraja Makafu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifurahia jambo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene muda mfupi baada ya kufungua kikao cha kwanza cha Bodi ya Ushauri ya LITA kilichofanyika jijini Dar es Salaam (25.07.2020)
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) akiteta jambo na
Kaimu Mkurugenzi wa Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene katika
kikao cha kwanza cha Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya LITA kilichofanyika jijini Dar
es Salaam. (25.07.2020)
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA), Prof. Malongo Mlozi (aliyesimama) akiongea na Wajumbe wa bodi hiyo wakati alipokuwa akiongoza kikao chao cha kwanza kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (25.07.2020)
Katibu Mkuu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na Wajumbe wa
Bodi Mpya ya Ushauri ya Wakala ya Vyuo vya Mifugo (LITA) wakati akifungua kikao
cha kwanza cha bodi hiyo kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (25.07.2020)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni