Katibu Mkuu Wizara ya
Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ameuelekeza uongozi unaosimamia
ujenzi wa kiwanda cha kusindika nyama cha Eliya kinachojengwa katika Wilaya ya
Longido Mkoani Arusha kuhakikisha unakamilisha ujenzi wa kiwanda hicho mapema
mwanzoni mwa mwaka 2020 ili kiweze kuleta tija kwa taifa na wafugaji wanaoishi
katika Mkoa wa Arusha, mikoa ya jirani na nchi ya jirani ya Kenya.
Prof. Gabriel amesema hayo
jana (24.10.2019) mara baada ya kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho akiwa pamoja
na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido na kukuta tayari ujenzi wa
kiwanda umefikia asilimia 90 ambapo mitambo mbalimbali imeanza kufungwa katika
kiwanda ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 kwa siku na mbuzi
takriban Elfu Mbili kwa siku.
Katibu mkuu huyo ametoa
wito kwa wadau wa mifugo kujipanga vizuri namna ya kutumia fursa ya uwepo wa
kiwanda hicho ili wafugaji na wafanyabiashara waweze kuuza mifugo katika
kiwanda hicho ambacho kitaongeza ajira na kukuza sekta ya mifugo nchini.
Awali akizungumza na wakuu
wa idara na vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Wilaya ya Longido kabla ya
kutembelea ujenzi wa kiwanda hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel amepokea maoni ya namna ya kudhibiti
vitendo vya kutorosha mifugo mipakani hali inayochangia kuikosesha serikali
mapato ambapo elimu imesisitizwa kwa watu wanaoishi mipakani.
Prof. Gabriel amesema
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inazidi kuchukua maoni ya namna ya kuhakikisha vitendo
vya utoroshaji wa mifugo hususan katika mpaka wa Namanga ambao ni kati ya
mipaka ya nchi za Tanzania na Kenya vinadhibitiwa ili kuhakikisha mapato ya
serikali hayapotei pamoja na kusimamia viwanda vya kusindika nyama kikiwemo cha
Eliya kinachotarajia kukamilika mapema mwaka 2020 kinapata mifugo ya kutosha
kutoka Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani ili kusindika nyama katika kiwanda
hicho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni