WASHIRIKI WA MAFUNZO YA UFUGAJI SAMAKI MKOANI KIGOMA WAMETAKIWA KWENDA KUZALISHA SAMAKI
Rai hiyo imetolewa 14 Septemba, 2026 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Bw. Hassan Rugwa Wakati akifunga mafunzo ya wiki nne kwa washiriki 57 wa mafunzo ya ufugaji samaki yaliyoendeshwa Mkoani Kigoma na Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Kigoma kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ubegiji Enabel kupitia mradi wa wezesha binti.
Bw. Rugwa amesema mafunzo waliopata washiriki hawa yawe chachu kwa wao kwenda kufanya shughui za uzalishaji, ufugaji na uchakataji wa samaki kwani Taifa linawategemea waweze kuongeza tija katika sekta ya ufugaji samaki.
Naye Mtendaji Mkuu wa FETA Dkt. Semvua Mzighani ambao ndio walioendesha mafunzo hayo amesema kuwa mafunzo haya ni kipaumbele cha Taifa kwa hivi sasa kwani serikali inaweka mkazo katika ukuzaji wa viumbe maji na ufugaji wa samaki.
Kwa upande wake Meneja wa FETA kampasi ya Kigoma Bw August Shirima amesema Mafunzo haya yalianza tarehe 17 Agosti mpaka tarehe 11 September 2026 ambapo washiriki kutoka Halmashauri ya kigoma vijijini na Manispaa ya kigoma Ujiji walipata mafunzo ya darasani kwa wiki mbili na mafunzo ya vitendo kwa wiki mbili.
Aidha amebainisha kuwa lengo ni kuwafikia washiriki 200 ambapo mpaka sasa washiriki 151 wameshafikiwa ambapo 84 ni wafugaji samaki na 67 ni wachakataji wa mazao ya samaki.
Naye Mwakilishi wa Enabel ambao ndio wafadhili wa mradi huu Bw. Magesa Mwangwa amesema wamefadhili mafunzo haya lengo kuwajengea uwezo vijana kuweza kujiajiri na kuajiriwa katika vituo mbalimbali vya ufugaji na uchakataji wa samaki.
Kwa upande wao washiriki waliopata mafunzo haya wameiomba serikali kuwawezesha mitaji ili waweze kujiajiri wenyewe katika sekta ya ufugaji samaki.
Mafunzo haya yataongeza uwezo wa vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa uvuvi na ukuzaji viumbe maji,kuongeza fursa za ajira na kujiajiri pamoja na kuwawezesha kuanzisha na kuendesha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki.







Maoni
Chapisha Maoni