WADAU WA FEDHA KUUNGA MKONO MRADI WA C-SDTP KUINUA SEKTA YA MAZIWA

Mradi wa Climate Smart Dairy Transformation Project (C-SDTP) unatarajiwa kuleta mabadiliko katika sekta ya maziwa nchini kwa kuongeza tija na kipato cha wafugaji, kuboresha maisha yao pamoja na kuongeza fursa za ajira.

Hayo yamebainika leo, Septemba 23, 2026, jijini Dodoma, katika kikao kazi kilichowakutanisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na wadau wa sekta ya fedha, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mradi huo, kuweka uelewa wa pamoja kuhusu mfumo wa ufadhili, kufafanua majukumu ya utekelezaji na taratibu za uendeshaji, pamoja na kukubaliana hatua za utekelezaji.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Stephen Michael, amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 na unalenga maeneo makuu matatu, ambayo ni kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa, kuongeza thamani ya mazao ya maziwa, pamoja na kuimarisha upatikanaji wa huduma za fedha na mikopo kwa wadau wa sekta hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Mikopo kutoka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB), Amani Shabani, amesema benki hiyo iko tayari kushirikiana katika utekelezaji wa mradi huo kwa kuwafikia wafugaji na kuwajengea uwezo benki washirika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kufikia malengo ya mradi.

Naye Meneja Mahusiano, Idara ya Stability kutoka Benki ya CRDB, Paul Kapu Makinya, amesema kupitia dhana ya Climate Smart, benki hiyo itasaidia kuendeleza uzalishaji unaozingatia uhifadhi wa mazingira, ikiwa ni pamoja na kusaidia katika uboreshaji wa miundombinu na kuwawezesha wazalishaji kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Mwakilishi kutoka Mfuko wa Kukuza Sekta ya Kifedha Tanzania (FSDT), Julia Seifert, amesema FSDT inaangalia namna bora ya kushirikiana na SACCOS zilizopo katika maeneo ya mradi ili kuhakikisha wafugaji wanapata huduma za kifedha kwa masharti nafuu na yanayowawezesha kuwekeza katika shughuli za uzalishaji wa maziwa.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI