TDB YAWEKA WAZI FURSA NA MWELEKEO WA TASNIA YA MAZIWA NCHINI
Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) imeweka wazi fursa na mwelekeo wa Tasnia ya Maziwa nchini, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Chakula, Mifugo na Ufugaji wa Kuku kwa Mustakabali 2026 yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
TDB imetoa elimu hiyo Septemba 03, 2026 kupitia mkutano uliofanyika sambamba na maonesho hayo katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, uliopo katika Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, ambapo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mipango wa TDB Bw. Cletus Shengena, akimwakilisha Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania, Prof. George Msalya, aliwasilisha mada yenye kichwa “Taswira ya Tasnia ya Maziwa Tanzania”
Katika mada hiyo, TDB iliainisha hali ya Tasnia ya Maziwa nchini pamoja na fursa zilizopo katika maeneo mbalimbali ikiwemo uzalishaji, ukusanyaji, uchakataji, uongezaji thamani na masoko ya bidhaa za maziwa.
Aidha, washiriki walipata fursa ya kufahamu maeneo muhimu yanayohitaji uwekezaji, ubunifu na matumizi ya teknolojia ili kuongeza tija na ushindani wa Tasnia hiyo.
Akizungumza katika mkutano huo, Bw. Shengena alisisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wadau wa Tasnia ya Maziwa katika kukabiliana na changamoto zilizopo na kutumia fursa zinazojitokeza kwa ajili ya kukuza uzalishaji na kuongeza thamani ya maziwa nchini.
Ushiriki wa TDB katika maonesho hayo ni sehemu ya utekelezaji wa jukumu lake la kuendeleza na kukuza Tasnia ya Maziwa nchini kwa kutoa elimu, kuhamasisha uwekezaji na kuwaunganisha wadau.
Pia, maonesho hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, teknolojia na taarifa zinazolenga kuimarisha uzalishaji wa chakula na mifugo kwa mustakabali wa Taifa.
Kupitia ushiriki huo, TDB imeendelea kusisitiza nafasi ya Tasnia ya Maziwa katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe, kuongeza kipato kwa wafugaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Tanzania.\




Maoni
Chapisha Maoni