TANZANIA KUONGEZA NGUVU KUTOKOMEZA SOTOKA YA MBUZI NA KONDOO

Tanzania imeendelea kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Sotoka ya Mbuzi na Kondoo (Peste des Petits Ruminants - PPR) kwa kutengeneza Mpango Mkakati wa hadi mwaka 2030, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda na nchi jirani katika kudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa huo unaoathiri mifugo na maisha ya wafugaji, hatua itakayoiweka Tanzania katika mstari wa mbele barani Afrika katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo unaodhuru mifugo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Mkutano wa Kikanda wa PPR uliofanyika leo Septemba 16, 2026 Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mikutano wa White Sands Resort, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, amesema Mpango huo ni wa kimkakati na ushirikiano wa nchi hizo ni hatua muhimu katika kukabiliana na magonjwa ya mifugo yanayovuka mipaka ya nchi.

Mhe. Kamani, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika mkutano huo akimwakilisha Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, amesema Tanzania imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali za magonjwa ya mifugo yanayosababisha vifo vya mifugo, hasara za kiuchumi na kukwamisha upatikanaji wa masoko ya kikanda na kimataifa, tatizo ambalo linaathiri usalama wa chakula, kipato cha kaya, na uchumi wa wafugaji wanaoishi katika maeneo ya mipakani, ndiyo maana Umoja wa Afrika pamoja na jumuiya ya kimataifa wamejitolea kuhakikisha ugonjwa huo unafutwa kabisa duniani ifikapo mwaka 2030.

 “Kulingana na vipimo vya kina vya maabara kwa ugonjwa wa PPR, kiwango cha uwepo wa kinga mwilini kiliongezeka kutoka asilimia 11.89 kabla ya chanjo hadi asilimia 89.25 baada ya chanjo, mabadiliko haya yanaonyesha ongezeko kubwa la uwiano wa mifugo iliyopimwa na kuonekana kuwa na kinga baada ya chanjo, na inaashiria kuwa mpango huu una uwezo wa kutokomeza ugonjwa wa PPR ifikapo mwaka 2030” amesema Mhe. Kamani.

Amesema udhibiti wa PPR unahitaji juhudi za pamoja, ikiwemo kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, utoaji wa chanjo, kubadilishana taarifa na utaalamu, pamoja na kuchukua hatua za haraka pale ugonjwa unapobainika, na Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi jirani pamoja na wadau wa sekta ya mifugo ili kuhakikisha hatua zinazochukuliwa katika kudhibiti PPR zinafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia mikakati ya kikanda na kimataifa ya kutokomeza ugonjwa huo.

Serikali zitaendelea kuimarisha ufuatiliaji unaozingatia tathmini ya hatari na uwezo wa maabara, ili kuendeleza udhibiti madhubuti kulingana na mpango wa kimkakati wa kitaifa, na kushirikiana kwa nia njema na majirani zetu katika usimamizi wa pamoja wa eneo hili la kinga, na itarahisisha usafiri wa timu za kitaalamu, kubadilishana taarifa za epidemiolojia na kuratibu shughuli za chanjo katika wilaya za mipakani, kwani majukumu haya yanachukuliwa kwa uzito mkubwa, kwa sababu afya ya mifugo inategemea maamuzi yanayofanywa vijijini pande zote mbili za mpaka, na si yale yanayofanywa katika mji mkuu pekee.

Pia amewashukuru kwa dhati kwa uungaji mkono endelevu Ofisi ya Umoja wa Afrika ya Rasilimali za Mifugo (AU-IBAR), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Sekretarieti ya SADC na washirika wa maendeleo, ambao msaada wao wa kitaalam na kifedha umewezesha mpango huu, na Tanzania inathamini sana ushirikiano huo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (kulia), akizungumza na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Nchini Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tipo (kushoto), kabla ya kuhitimisha Mkutano wa Kikanda wa kuandaa Mkakati wa kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa sotoka ya Mbuzi na kondoo (PPR) uliyojumuisha nchi tatu ikiwemo Tanzania, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa White Sands Resort, Septemba 16, 2026 Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (aliyesimama), akihutubia wadau wa sekta ya mifugo kutoka nchi mbalimbali, katika kuhitimisha Mkutano wa Kikanda wa kuandaa Mkakati wa kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa sotoka ya Mbuzi na kondoo (PPR) uliyojumuisha nchi tatu ikiwemo Tanzania, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa White Sands Resort, Septemba 16, 2026 Dar es Salaam.

Picha ni wadau wa sekta ya mifugo kutoka nchi tatu, wakimsikiliza  Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (hayupo pichani), katika kuhitimisha Mkutano wa Kikanda wa kuandaa Mkakati wa kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa sotoka ya Mbuzi na kondoo (PPR) uliyojumuisha nchi tatu ikiwemo Tanzania, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa White Sands Resort, Septemba 16, 2026 Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (aliyekaa katikati mstari wa mbele), akiwa katika picha ya pamoja na wadau kutoka nchi mbalimbali wa sekta ya mifugo, katika kuhitimisha Mkutano wa Kikanda wa kuandaa Mkakati wa kudhibiti na kutokomeza ugonjwa wa sotoka ya Mbuzi na kondoo (PPR) uliyojumuisha nchi tatu ikiwemo Tanzania, Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa White Sands Resort, Septemba 16, 2026 Dar es Salaam.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI