SHAMBA LA MIFUGO SAO HILL KUEKEWA MIFUMO YA UMWAGILIAJI

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, amesema mpango wa kujenga miundombinu ya maji kwa ajili ya umwagiliaji katika Shamba la Kuzalisha Mifugo la Sao Hill, lililopo Mafinga, mkoani Iringa, unatakiwa kuharakishwa na kuwaagiza wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, iliyo chini ya Wizara yake, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kufanya tathmini kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hatua hiyo imekuja wakati Mhe. Chongolo, akiwa na mwenyeji wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa, walipotembelea na kukagua vyanzo vya maji katika Shamba la Mifugo la Serikali la Sao Hill leo, Septemba 12, 2026, ambapo Mawaziri hao wamekubaliana kushirikiana kwa lengo la kuleta mapinduzi katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.

Lengo la kuweka miundombinu ya maji katika shamba hilo ni kuhakikisha wafugaji wanapata malisho ya uhakika na kufanya ufugaji wenye tija, hatua ambayo itasaidia kupunguza tabia ya kuvamia mashamba ya kilimo cha mazao na hivyo kupunguza migogoro kati ya wafugaji na wakulima.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally, akizungumzia ushirikiano kati ya Wizara yake na Wizara ya Kilimo, amesema wamekubaliana kushirikiana katika kilimo cha malisho, hasa kwa kuweka miundombinu wezeshi ya maji kwa ajili ya umwagiliaji na kunyweshea mifugo, ambapo pia alibainisha mahitaji ya kuzingatiwa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa unaolenga kuwainua wafugaji wadogo kuwa ni uhakika wa eneo la malisho na maji, mbegu bora, afya ya mifugo, miundombinu, mitaji na masoko.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Selekwa, amesema Halmashauri za Mji Mafinga na Mufindi zimekuwa zikitoa kipaumbele katika fedha za asilimia 10 kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake kufanya ufugaji na kilimo cha mboga mboga, ili kuhakikisha wanazalisha protini kwa wingi na kukabiliana na udumavu ambapo hadi sasa, jumla ya Shilingi bilioni 2 zimetolewa na halmashauri hizo mbili.

Naye, Mbunge wa Mafinga Mjini, Mhe. Dickson Lutevele, na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Mhe. Emanuela Kaganda, wamepongeza hatua hiyo ya Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ya kuanza kushirikiana, wakisema ushirikiano huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha sekta za kilimo na mifugo, ikiwemo Shamba la Sao Hill.


Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (wa tatu kulia), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally (wa kwanza kushoto) na baadhi ya wataalam wa Wizara za Kilimo, Mifugo n Uvuvi wakagua miundombinu ya kunyweshea mifugo maji katika shamba la Sao Hill, Septemba 12, 2026.

Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (kulia), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally (kushoto)  na wataalam wa Wizara za Kilimo, Mifugo n Uvuvi wakagua miundombinu ya kunyweshea maji mifugo katika shamba la Sao Hill, Septemba 12, 2026.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally na Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo wakifurahia pamoja baada kufika katika shamba la mifugo la Sao Hil kwa Lengo la Kuangalia miundombinu ya shamba hilo kwa ajili uwekaji wa mifumo ya maji




Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI