SERIKALI YATAKA TEKNOLOJIA NA UWEKEZAJI KULETA MAPINDUZI SEKTA YA MIFUGO

Serikali imetoa wito kwa wadau wa sekta ya mifugo kuongeza matumizi ya teknolojia, ubunifu na uwekezaji ili kuongeza uzalishaji, tija na thamani ya bidhaa za mifugo, hatua inayolenga kuleta mapinduzi katika sekta hiyo nchini.

Wito huo umetolewa Septemba 02, 2026 na Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Steven Michael, wakati akifungua Mkutano wa Tatu wa Chakula, Mifugo na Ufugaji wa Kuku kwa Mustakabali 2026, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ali Kakurwa, katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Bw. Michael amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia na ubunifu katika kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mifugo, pamoja na kuimarisha mnyororo wa thamani kuanzia uzalishaji hadi masoko. 

Ameeleza kuwa sekta ya mifugo ina mchango mkubwa katika usalama wa chakula na lishe, ajira, kipato cha wananchi na ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Akizungumzia tasnia ya kuku, Bw. Michael amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi, hatua hiyo inaenda sambamba na uzinduzi wa Mkakati wa Kukuza Tasnia ya Kuku, uliozinduliwa na Waziri Mkuu Mhe. Mwigulu Nchemba wakati akifungua Maonesho ya Nanenane yaliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema mkakati huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uzalishaji wa kuku na bidhaa zake, kuongeza tija, kuendeleza mnyororo wa thamani na kufungua fursa zaidi za masoko na uwekezaji kwa wafugaji na wadau wa tasnia ya kuku.

Aidha, amewataka wadau kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa sekta ya mifugo kwa kuongeza uwekezaji katika uzalishaji, uchakataji, uongezaji thamani na masoko ya bidhaa za mifugo.

Kwa upande wa Tasnia ya Maziwa, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uzalishaji na uchakataji ili kuongeza upatikanaji wa bidhaa bora na salama za maziwa na kuongeza kipato kwa wafugaji.

Bw. Michael pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wafugaji, wataalamu na wadau wa maendeleo katika kutatua changamoto zilizopo na kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana katika sekta ya mifugo na kuku.

Mkutano huo umefanyika sambamba na Maonesho ya Chakula, Mifugo na Ufugaji wa Kuku kwa Mustakabali 2026, ukiwakutanisha wadau mbalimbali kujadili fursa, changamoto, teknolojia na ubunifu katika sekta ya chakula, mifugo na ufugaji wa kuku, kwa lengo la kujenga mifumo ya uzalishaji yenye tija na endelevu.

Hatua hizo zinaendelea kuimarisha nafasi ya sekta ya mifugo na kuku katika kuchochea uzalishaji wa chakula, kuongeza ajira na kipato, pamoja na kuchangia utekelezaji wa malengo ya Taifa kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Mkurugenzi wa Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Bw. Steven Michael, akifungua mkutano wa Tatu wa Chakula, Mifugo na Ufugaji wa kuku kwa Mustakabali wa 2026 kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, uliofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Viwanja vya Sabasaba, jijini Dar es Salaam Septemba 02, 2026 ambapo umewakutanisha wadau mbalimbali kujadili fursa, ubunifu na maendeleo ya sekta ya chakula, mifugo na ufugaji wa kuku nchini.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI