MHE. KAMANI AWATAKA TVLA KUSIMAMIA UBORA WA VYAKULA VYA MIFUGO

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, ameitaka Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kuimarisha usimamizi wa ubora wa vyakula vya mifugo vinavyozalishwa na kampuni mbalimbali nchini, ili kuhakikisha vinakidhi viwango na vigezo vinavyotakiwa.

Mhe. Kamani ameyasema hayo leo, Septemba 18, 2026, jijini Dar es Salaam, alipofanya ziara katika Shamba la Kuku la Harvest Point Limited, linalojishughulisha na uzalishaji wa kuku wa mayai, chakula cha kuku pamoja na kutoa huduma za ugani kwa wafugaji.

Amesema TVLA inapaswa kuhakikisha viwanda vinavyozalisha vyakula vya mifugo vinakaguliwa na kusimamiwa ipasavyo, sambamba na kutoa elimu na ushauri kwa wataalamu wa viwanda hivyo, ili kuhakikisha chakula kinachozalishwa kinakuwa na ubora unaokidhi mahitaji ya mifugo.

“Ni muhimu TVLA kuhakikisha mnakagua viwanda hivi na kuwapatia wataalamu wake elimu ya kutosha, ili chakula kinachozalishwa kiwe bora na kiweze kumsaidia mfugaji kuongeza uzalishaji,” amesema Mhe. Kamani.

Aidha, amewataka wawekezaji katika sekta ya mifugo na uvuvi kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha na kuendelea kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu mbinu bora za uzalishaji, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi nchini.

Vilevile, Mhe. Kamani amesema Serikali inaendelea na juhudi za kurasimisha na kuimarisha tasnia ya kuku nchini, ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Tasnia ya Kuku ambao tayari umezinduliwa.

Amesema mpango huo unalenga kukuza tasnia ya kuku na kuongeza fursa za kiuchumi, hususan kwa wanawake na vijana, pamoja na kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hiyo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kamani pia alitembelea Kampuni ya Tanlapia Limited, inayojishughulisha na ukuzaji wa viumbe maji kwa njia ya mabwawa, na ameipongeza kampuni hiyo kwa kutoa ajira kwa vijana pamoja na kutoa huduma za ugani kwa wafugaji, ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikitolewa na Wizara, akieleza kuwa ushiriki wa sekta binafsi katika utoaji wa huduma hizo ni muhimu katika kuongeza ufanisi na kuwafikia wafugaji wengi zaidi.

Mhe. Kamani ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za ugani zinatolewa kwa weledi na ufanisi, kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuimarisha maendeleo ya sekta ya mifugo na uvuvi nchini.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (wa pili kushoto), akielezewa ubora wa teknolojia inayotumiwa na Kampuni ya Tanlapia Limited katika ukuzaji viumbemaji, na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Baraka Karangahe (wa pili kulia), mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 18, 2026 Bagamoyo - Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (wa kwanza kushoto), akikagua miundombinu ya shamba la kuku la Harvest Point Limited, mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 18, 2026 Bagamoyo - Jijini Dar es Salaam, wa kwanza kulia ni na Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Bw. Fadhili Gwota.









Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI