MHE. KAMANI AWAONESHA FURSA WAWEKEZAJI SEKTA YA MIFUGO NA UVUVI

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amewataka wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa zilizopo katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, akiahidi ushirikiano wa Serikali katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki na wezeshi.

Mhe. Kamani ametoa kauli hiyo leo, Septemba 17, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara maalum ya kikazi ya kutembelea wawekezaji wanaofanya shughuli katika Sekta za Mifugo na Uvuvi.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri ametembelea Kampuni ya Alphakrust Limited pamoja na Kampuni ya Farmbase, ambapo amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji zinazofanyika katika sekta hizo.

Amesema Serikali imedhamiria kushirikiana kwa karibu na Sekta binafsi katika kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Kamani amesema Serikali inaendelea kuweka mifumo inayorahisisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi, ili kuongeza uzalishaji, kuchochea uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta hizo katika uchumi wa Taifa.

Aidha, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 unalenga kuongeza nafasi ya Sekta binafsi katika kujenga uchumi wa Taifa, ambapo Serikali imejipanga kushirikiana na wawekezaji kufikia malengo hayo.

“Serikali ipo bega kwa bega na Sekta binafsi kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuwa rafiki na wezeshi,” amesema Mhe. Kamani.

Amebainisha kuwa Tanzania ina fursa nyingi katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, huku akiwataka wawekezaji kuzitumia fursa hizo katika kuongeza uzalishaji na thamani ya bidhaa zinazotokana na sekta hizo.

Mhe. Kamani pia ametoa shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji, ikiwemo upatikanaji wa ardhi, mitaji pamoja na mifumo ya kodi inayolenga kuwezesha uwekezaji nchini.

Amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi utaendelea kuwa nguzo muhimu katika kukuza Sekta za Mifugo na Uvuvi na kuongeza manufaa yake kwa Taifa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (aliyeshika kopo la dawa), akitazama bidhaa iliyozalishwa na Kampuni ya Farmbase Limited, mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 17, 2026 Jijini Dar es Salaam, wa kwanza kushoto ni na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Farmbase Limited, Bw. Suleiman Msellem.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (wa Tano kushoto), akimsikiliza Meneja wa uzalishaji Kampuni ya Alphakrust Limited, Bw. Sreejith kasavan (wa tatu kushoto), akielezea namna uchakataji wa pweza unavyofanyika, mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 17, 2026 Jijini Dar es Salaam, wa sita kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo, Bw. Sunny Solanki.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (kulia), akikabidhiwa tuzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Farmbase Limited, Bw. Suleiman Msellem (kushoto), mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 17, 2026 Jijini Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (anayepanda mti), akipanda mti nje ya eneo la Kampuni ya Farmbase Limited kama ishara ya kuwatakia mema Kampuni hiyo, mara baada ya kuwasili kwenye Kampuni hiyo ili kujionea shughuli za uzalishaji, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kuwatembelea wawekezaji katika Sekta za Mifugo na Uvuvi, Septemba 17, 2026 Jijini Dar es Salaam.








Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI