MHE. KAMANI AITAKA TADB KUENDELEA KUTOA MIKOPO NA KUFANYA UFUATILIAJI WA KINA KWA WANUFAIKA WA MRADI WA BBT

◾ Aitaka TADB kuanzisha Mfumo wa Taarifa za Wanufaika.

◾ Aitaka TADB kuendelea kutoa mikopo kwa vijana.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, ameitaka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kuendelea kutoa mikopo kwa vijana wanaonufaika wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) Mifugo na Uvuvi, huku ikifanya ufuatiliaji wa kina na tathmini ya miradi inayotekelezwa ili kuhakikisha mikopo hiyo inaleta tija na matokeo yaliyokusudiwa.

Mhe. Kamani ametoa agizo hilo leo, Septemba 12, 2026, jijini Mwanza, alipofanya ziara maalum ya kikazi katika Ofisi ya TADB Kanda ya Ziwa, ziara ambayo ni sehemu ya siku tatu za ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa.

Katika ziara hiyo, Mhe. Kamani ameitaka TADB kuhakikisha inapatikana takwimu sahihi kuhusu idadi ya vijana wanaonufaika na Mradi wa BBT pamoja na thamani ya miradi yao, hatua ambayo itasaidia Serikali kupima mafanikio ya programu hiyo na kufanya maboresho yanayohitajika.

Amesema ufuatiliaji na tathmini ya miradi hiyo ni muhimu katika kuhakikisha vijana wanapata tija inayotarajiwa, jambo ambalo litasaidia kujenga imani na kuwawezesha vijana wengine kunufaika na mikopo hiyo kwa wingi zaidi.

“Miradi hii ya Serikali isikopewe na Taasisi yoyote, ili kuweza kurahisisha marejesho na kutopoteza fedha za Umma kiurahisi,” amesema Mhe. Kamani.

Aidha, Mhe. Kamani ameitaka TADB kuendelea kutoa mikopo kwa vijana wanaojihusisha na shughuli za vizimba, ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kujenga kipato endelevu kupitia shughuli za uvuvi.

Pamoja na hilo, ameitaka TADB kuanzisha Mfumo wa Taarifa utakaowezesha kuhifadhi na kutoa taarifa muhimu kuhusu mikopo inayotolewa pamoja na taarifa za vijana wanaonufaika na programu ya BBT.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa Mwanza, Bw. Charles Mbelwa, amesema mfumo huo unatarajiwa kuwa tayari na kuanza kufanya kazi ifikapo Desemba mwaka huu.

Amesema mfumo huo utasaidia kuweka kumbukumbu muhimu na takwimu sahihi za wanufaika, hivyo kurahisisha ufuatiliaji na tathmini ya miradi inayotekelezwa kupitia mikopo hiyo.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani, akizungumza na Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Kanda ya Ziwa (hawapo pichani), mara baada ya kupokea Taarifa ya utekelezaji wa Utoaji Mikopo kwa Vijana wanufaika wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kikao kilichofanyika katika Ofisi za TADB Kanda ya Ziwa, wakati wa ziara yake ya kikazi Jijini Mwanza, Septemba 12, 2026.

Kaimu Meneja Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Kanda ya Ziwa, Bw. Charles Mbelwa, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (hayupo pichani) kuhusu Utekelezaji wa ujumla wa TADB katika kuwawezesha mikopo kwa vijana, wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo Jijini Mwanza, kikao kilichofanyika katika Ofisi za TADB Kanda ya Ziwa, Septemba 12, 2026.

Afisa Masoko Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Kanda ya Ziwa, Bi. Glacia Marugujo (wa pili kulia), akitoa taarifa ya utekelezaji wa Utoaji Mikopo kwa Vijana wa Mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) Mifugo na Uvuvi kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (wa kwanza kushoto), wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo Jijini Mwanza, kikao kilichofanyika katika Ofisi za TADB Kanda ya Ziwa, Septemba 12, 2026.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani (katikati), akiwa kwenye picha ya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Watendaji wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza na Watendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB) Kanda ya Ziwa, mara baada ya kikao kifupi, kilichofanyika katika Ofisi za TADB Kanda ya Ziwa, wakati wa ziara yake ya kikazi Jijini Mwanza, Septemba 12, 2026.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI