KAMANI AKUTANA NA WATAALAM KUJADILI MAENDELEO YA SEKTA YA MIFUGO
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng’wasi Damas Kamani, amekutana na wataalamu kutoka Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko (DPMD) na Idara ya Huduma za Mifugo (DVS), kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa pamoja na majukumu mbalimbali yanayotekelezwa na idara hizo.
Vikao vyote vilivyomkutanisha Naibu Waziri Mhe. Kamani pamoja na wataalam kutoka vitengo na idara hizo vilifanyika leo Agosti 31, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kambarage Tower, jijini Dodoma kwa nyakati tofauti.
Katika kikao na wataalamu wa ICT, Mhe. Kamani alipokea taarifa na kushuhudia maonesho ya mfumo (demonstration) utakaotumika katika zoezi la utoaji wa mikopo kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi, ambapo baada ya kupitia mfumo huo, alitoa mapendekezo na maelekezo mbalimbali kwa ajili ya kuuboresha kabla ya kuanza kutumika.
Katika hatua nyingine, kikao na wataalamu wa Idara ya Uzalishaji na Maendeleo ya Masoko, Mhe. Kamani alijadiliana nao juu ya namna ya kubuni na kuanzisha mfumo bora wa kukusanya mapato katika minada ya mifugo, hatua inayolenga kudhibiti na kuondokana na upotevu wa mapato.
Kwa upande wa Idara ya Huduma za Mifugo (DVS), Mhe. Kamani na wataalam wa idara hiyo walijadilina kuhusu suluhisho linalotekelezeka (practical solution) la kuongeza tija katika Sekta ya Mifugo nchini ikiwa ni pamoja na kubaini sababu zinazoathiri uzalishaji na tija katika sekta hiyo, pamoja na kuweka hatua mahsusi za kukabiliana na changamoto hizo na kuboresha hali ya Sekta ya Mifugo nchini.






Maoni
Chapisha Maoni