KAMANI AITAJA MIKAKATI KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA SAMAKI ZIWA TANGANYIKA

DODOMA: Serikali imesema wingi wa samaki katika Ziwa Tanganyika umepungua kwa asilimia 62, kutoka tani 304,500 mwaka 1998 hadi kufikia takribani tani 116,000 mwaka 2026. 

Hayo yamesemwa leo Septemba Mosi 2026 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Ng'wasi Damas Kamani wakati akijibu swali la Mbunge wa Kalambo, Mhe. Edifonsi Joakim Kanoni, aliyetaka kujua lini Serikali itafanya utafiti wa kubaini wingi wa samaki katika ziwa hilo.

Mhe. Kamani amesema Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) hufanya tafiti za kubaini wingi na mtawanyiko wa samaki wa tabaka la juu (pelagic species) kwa kushirikiana na nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia huku kwa upande wa Tanzania, tafiti hizo zilifanyika mwaka 1998, 2022 na 2024, huku utafiti wa mwaka 2025 na 2026 ukifanyika kwa ushirikiano wa nchi hizo.

"Matokeo yanaonesha mwenendo wa kupungua kwa rasilimali za samaki, hususan dagaa na migebuka, hali inayolazimu kuimarishwa kwa ulinzi wa mazalia na udhibiti wa uvuvi usiozingatia sheria. Serikali pia inaendelea kuendeleza teknolojia ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba ili kuongeza uzalishaji" alisema Mhe. Kamani.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushiriki katika kulinda rasilimali na mazalia ya samaki pamoja na kuzingatia sheria za uvuvi na kwamba  Serikali inakamilisha mchakato wa kuunda Mamlaka ya Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi na udhibiti wa rasilimali hizo.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

SHAMBA LA KITULO KUWA KITOVU CHA NG’OMBE BORA WA MAZIWA NCHINI