FETA YAZINDUA MAFUNZO YA UZALISHAJI WA VIFARANGA VYA SAMAKI MOROGORO NA MWANZA

Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) kwa ufadhili wa Shirika la World Fish tarehe 23 Septemba, 2026 imezindua mafunzo ya siku 4 kuhusu uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya Sato na Kambale Mkoani Morogoro na Jijini Mwanza.

Mafunzo haya yamehusisha washiriki 54 ambapo 30 wanapatiwa mafunzo katika Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji Kingolwira, Morogoro na washiriki 24 wanapatiwa mafunzo Kampasi ya FETA Nyegezi, Mwanza.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Ukuzaji Viumbe Maji Wizara ya Mifugo na uvuvi, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Ukuzaji Viumbe Maji Bi Janeth Rukanda amesema mahitaji ya vifaranga bora vya samaki ni makubwa kulingana nahali ya uzalishaji wa sasa na ukuaji wa teknolojia. Hivyo mafunzo haya ni msingi endelevu wa utakaowezesha kuzalisha vifaranga bora na vya kutosha.

"Tunatarajia baada ya mafunzo haya tutaongeza upatikanaji wa vifaranga bora vya samaki pamoja na kusambaza teknolojia ya  utotoleshaji ili kuendana na ukuaji wa teknolojia" Amesema Bi Rukanda.

Naye Naibu Mkuu wa FETA Bi Merisia Mparazo  kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa FETA amesema  kuwa mafunzo haya yana umuhimu mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya  Taifa 2050 ambayo inasisitiza kujenga uchumi wenye tija, ushindani, na utengenezaji wa ajira  kwa wananchi kupitia sekta zalishaji ikiwemo Sekta ya Uvuvi.

Aidha, amewashukuru Worldfish kwa kuendelea kushirikiana na Feta kutekeleza masuala mbalimbali ikiwemo kuwezesha  mafunzo haya yanayokwenda kuleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya ufugaji samaki.

Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo haya Bw Mashaka Kapagalla amesema kuwa mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo yaliyofanyika Kampasi ya FETA Mbegani mwezi Februari 2026 na kuhusisha washiriki 32 kupitia ufadhili wa Worldfish chini ya Mradi wa Fish Compact. Lengo la mradi ni kuwafikia washiriki 1,500 nchini ambapo hadi sasa washiriki 86 wamefikiwa.

Washiriki  wanapatiwa ujuzi wa utunzaji wa samaki wazazi, uzalishaji na utunzaji wa vifaranga vya samaki pamoja na usimamizi wa vitotoleshi vya samaki aina ya Sato na Kambale.






Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

WATAALAMU WATAKIWA KUKUSANYA TAKWIMU SAHIHI ZA KITAFITI

TANZANIA DAIRY BOARD

LESENI, VIBALI VYA MAZAO YA MIFUGO NA VYAKULA VYA SAMAKI KUTOLEWA KWA NJIA YA KIELEKTRONIKI