FETA YAZINDUA MAFUNZO YA MUDA MFUPI JUU YA UONGOZI WA JAMII KATIKA UHIFADHI WA RASILIMALI ZA BAHARI NA PWANI
Wakala ya Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA) Kampasi ya Mbegani leo 14 Septemba, 2026 imezindua mafunzo ya muda mfupi ya uongozi wa jamii katika uhifadhi wa rasilimali za Bahari na Pwani, yanayolenga kuwajengea uwezo viongozi wa jamii 20 kutoka Tanga na Pemba.
Mafunzo hayo yalioanza tarehe 14 hadi 27 Septemba 2026, yanafadhiliwa na shirika la IUCN Tanzania ambapo yatahusisha maeneo muhimu yakiwemo uongozi, utawala bora, usimamizi wa fedha, mawasiliano na ushirikiano wa wadau, sera na sheria, utatuzi wa migogoro, utetezi wa maslahi ya jamii na uibuaji wa shughuli mbadala za kuongeza kipato.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Capt. Nicas Mbandi aliyemwakilisha Naibu Mkuu wa FETA, amesisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi wenye maarifa na ujuzi wa kusimamia rasilimali za Bahari kwa kuunganisha uhifadhi na maendeleo ya jamii.
Aidha amesema mafunzo haya yanachangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuwekeza katika watu wenye ujuzi na uwezo wa kuongoza, pamoja na kukuza uchumi wa buluu, ajira, kipato na matumizi endelevu ya rasilimali za Bahari na Pwani.
Pia amewahimiza washiriki kutumia maarifa watakayoyapata kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao na kuwa mawakala wa mabadiliko katika uhifadhi na maendeleo endelevu ya rasilimali za Pwani na Bahari huku akitoa shukrani kwa IUCN Tanzania kwa kufadhili mafunzo hayo na kusisitiza dhamira ya kuendeleza ushirikiano katika kujenga uwezo wa jamii na wadau wa sekta ya uvuvi na uhifadhi wa rasilimali za Pwani na Bahari.



Maoni
Chapisha Maoni